1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken aiambia Urusi kuruhusu nafaka ya Ukraine nje

8 Julai 2022

Marekani na washirika wake wa Magharibi wameishinikiza Urusi kuhusu vita vyake ambavyo havikuchochewa nchini Ukraine wakati wa mkutano wa kundi la mataifa tajiri na yanayoinukia G20 nchini Indonesia .

https://p.dw.com/p/4DqtX
USA Washington | Pressekonferenz: Antony Blinken und  Jens Stoltenberg
Picha: Jacquelyn Martin/AP/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov Ijumaa walijiunga na wenzao wa kundi hilo la G20 kwa mazungumzo ya siku nzima huu ukiwa mkutano wa kwanza tangu kuzuka kwa vita vya Urusi nchini Ukraine huku mwenyeji wao akiwaambia mara moja kwamba mapigano hayo lazima yasitishwe kupitia mazungumzo.

Kabla ya mkutano huo katika mji wa mapumziko wa Bali, Blinken alikutana na wenzake wa Ujerumani na Ufaransa  na afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Uingereza kuzungumza kuhusu uvamizi huo wa Urusi nchini Ukraine. Haya ni kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa mawaziri hao walitathmini upya njia za kushughulikia wasiwasi wa usalama wa chakula duniani unaotokana na hatua ya Urusi kulenga kwa makusudi sekta ya kilimo ya Ukraine .

Baadaye wakati wa kikao cha pamoja cha mkutano huo wa G20 ambacho kilikuwa kinaangazia suala la ukosefu wa chakula na nishati, Blinken alisema kuwa  Urusi inapaswa kuruhusu nafaka ya Ukraine kusafirishwa kote duniani.

Iran | PK Sergej Lavrov
Sergey Lavrov - Waziri wa mambo ya nje wa UrusiPicha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Huku hayo yakijiri, Lavrov ameyashtumu mataifa ya Magharibi kwa kuihimiza Ukraine kutumia silaha na pia kuyashtumu mataifa hayo kwa kuifanya Urusi kuonekana kuwa taifa chokozi katika vita hivyo bila ya kutathmini ukweli ulioko. Lavrov pia alivishtumu vikwazo vya Magharibi dhidi ya Urusi tangu kuanza kwa vita hivyo mnamo mwezi Februari. Lavrov amesema, alihudhuria mkutano huo wa G20 kupata taswira ya jinsi mataifa ya Magharibi yanavyochukulia suala hilo.

Urusi iko tayari kuingia katika mazungumzo na Uturuki

Hata hivyo Lavrov amesema kuwa Urusi iko tayari kuingia katika mazungumzo na Uturuki kutafuta njia ya kuruhusu Ukraine kusafirisha nje bidhaa zake za nafaka. Ukraine ni mzalishaji na msambazaji muhimu wa nafaka katika sehemu nyingi za dunia; Lakini kutokana na vita hivyo na vizuizi katika bandari zake, kiwango kikubwa cha nafaka hakisafirishwi nje na kusababisha matatizo kote duniani.

Pia alishtumu vikwazo hivyo vya Magharibi na kusema tatizo la usambazaji wa chakula duniani sio kwasababu ya kupungua kwa bidhaa za Ukraine lakini kwasababu vikwazo vya kimataifa vinazuia mazao ya ngano ya Urusi.

i