1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Blinken afanya ziara ya kushtukiza Ukingo wa Magharibi

5 Novemba 2023

Ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken inalenga kusaka amani huko mashariki ya kati wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea huko Gaza.

https://p.dw.com/p/4YQDT
Blinken akutana na Abbas mjini Ramallah, Ukingo wa Magharibi
Blinken akutana na Abbas mjini Ramallah, Ukingo wa MagharibiPicha: PPO/AFP

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amefanya ziara ya kushtukiza yenye ulinzi mkali, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel na kukutana na rais wa Palestina Mahmud Abbas.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani alikutana na Abbas mjini Ramallah huku wasiwasi wa kimataifa ukiongezeka juu ya kuongezeka kwa ghasia katika eneo hilo kutokana na vita vya Israel na Hamas huko Gaza tangu Oktoba 7.

Blinken ameitembelea Israel tangu kuanza kwa vita, lakini hii ilikuwa ni safari yake ya kwanza katika Ukingo wa Magharibi.

Wakati hayo yakiarifiwa, maafisa wa usalama mjini Gaza wamesema ndege za kivita za Israel zimeishambulia kambi ya wakimbizi ya Maghazi mjini humo mapema leo asubuhi, na kusababisha mauaji ya watu 33 na wengine wengi kujeruhiwa.

Mashambulizi hayo yametokea wakati Israel ikisema itaendeleza mashambulizi yake ili kuusambaratisha kabisa utawala wa Hamas katika eneo hilo, licha ya ombi la Marekani la kutaka mapigano yasitishwe kwa muda, ili kutoa nafasi kwa misaada ya kiutu kuwafikia raia wa mji huo.

Miito wa kusitishwa mashambulizi

Ndege za kivita za Israel zaishambulia kambi ya wakimbizi Gaza
Ndege za kivita za Israel zaishambulia kambi ya wakimbizi Gaza Picha: Hatem Moussa/AP/picture alliance

Idadi ya vifo mjini Gaza iliyopindukia 9000 imesababisha hasira inayoendelea miongoni mwa raia wa mataifa ya nje huku maelfu ya waandamanaji wakimiminika barabarani mjini Berlin Ujerumani na hata Washington Marekani kutaka mapigano yasitishwe mara moja.

Waziri Mkuu wa Jordan Ayman Safadi amesema mataifa ya kiarabu yanataka mapigano yasitishwe haraka akisisitiza kuwa kanda nzima inazama katika bahari ya chuki itakayoathiri vizazi vijavyo.

Wakati huo huo, gazeti la The Times nchini Israel limeripoti kuhusu mamia ya raia nchini humo wamemtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ajiuzulu wakati walipoandamana nje ya nyumba yake mjini Jerusalem.

Polisi yatawanya waandamanaji

Polisi walijaribu kuwatawanya waandamanaji jana Jumamosi jioni na kuwakamata watu watatu, ikidai waandamanaji wamehatarisha usalama  nje ya nyumba ya Waziri Mkuu.

Waandamanaji hao walimtaka Netanyahu kuidhinisha mpango wa kubadilishana mateka wanaoshikiliwa mjini Gaza, wakimtuhumu kwa kushindwa katika majukumu yake na namna anavyoshughulikia majibu ya mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyofanywa Kusini mwa Israel na wanamgambo wa Hamas.

Maandamano mengine ya kumpinga Benjamin Netanyahu pia yalishuhudiwa katika miji mingine ya Tel Aviv, Haifa, Beersheba na Eilat.

Chanzo: reuters,afp