1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BLANTYRE : Rais wa Malawi yumkini kushtakiwa

22 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFUZ

Kundi la wabunge nchini Malawi linapanga kumshtaki Rais Bingu wa Mutharika baadae mwezi huu kwa madai kwamba amekiuka katiba ya nchi hiyo.

Mjadala wa kumshtaki rais huyo ulifanyika mwishoni mwa juma lililopita katika makao ya Rais wa zamani na kiongozi wa Chama cha United Demokratic Front UDF Bakili Muluzi ambaye yuko katika mfarakano wa wazi na Mutharika.

Kwa mujibu wa msemaji wa UDF Sam Mpasu zaidi ya wabunge 40 katika bunge lenye wabunge 193 walihudhuria mkutano huo.

Mpasu amesema Mutharika alikiuka katiba wakati alipoanzisha mchango wa mfuko wa dola milioni 100 kwa ajili ya wananchi maskini wa Malawi bila ya kuidhinishwa na bunge. Ukiukaji mwengine wa katiba anaoshutumiwa ni kumteuwa mkuu wa polisi bila ya idhini ya bunge.

Katika mzozo mkali na Muluzi Mutharika ametoka katika chama cha UDF kwa kusema kwamba amekuwa akiingiliwa kati kisiasa na rais huyo wa zamani ambaye bado ana madaraka mengi ndani ya chama hicho.