1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uinmgereza Yashinikizwa

28 Juni 2016

Viongozi 27 wa Umoja wa ulaya wapania kutuliza hofu miongoni mwa wakaazi wa Ulaya na walimwengu kufuatia kura ya maoni ya Uingereza Brexit. Kansela Angela Merkel amezungumzia kadhia ya Brexit bungeni mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/1JEsi
Kansela Angela Merkel (Kati) na rais Francois Hollande wa Ufaransa(kushoto) na waziri mkuu wa Italy Matteo Renzi wakizungumza na waandishi habari mjini BerlinPicha: Reuters/H. Hanschke

Viongozi wa taifa na serikali za Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Bruxelles wanapanga kuihimiza Uingereza ianzishe utaratibu wa kujitoa bila ya kupoteza wakati ili kuepukana na balaa katika masoko ya hisa huku wakijifunza kutokana na kura ya maoni ya Brexit na kuepusha yaliyotokea Uingereza yasitokee kwengineko .

Mkutano huo utakaoanza leo usiku utampatia fursa waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ya kujieleza."Kuna mambo yatakayojitokeza wakati wa majadiliano hayo: kuzingatia matokeo ya kura ya maoni,kushadidia ule ukweli kwamba katika hali kama hii,Makubaliano ya Lisbone yanatoa mwongozo wa kisheria unaobidi kufuatwa, mwongozo uliofafanuliwa katika kifungu nambari 50 kinachozungumzia kuhusu"kujitoa" amesema mwanadiplomasia mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe.

Kesho,wakati wa karamu ya asubuhi mwenyekiti wa baraza la Ulaya Donald Tust atakutana na viongozi 27 wa Umoja wa Ulaya,bila ya David Cameron ili kuzungumzia matokeo ya kujitenga Uingereza na mustakbali wa uhusiano pamoja na nchi hiyo.

Uingereza isitegemee kufaidika bila ya kuwajibika

Wakati huo huo mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker ameisihi Uingereza ifafanue haraka hali ya mambo baada ya kura ya Brexit."Hatuwezi kuendelea na hali isiyokadirika. Nnataka Uingereza ifafanue msimamo wake,si leo si kesho bali haraka iwezekanavyo" amesisitiza Jean Claude Juncker mbele ya wabunge wa Ulaya mjini Bruxelles."Hakuna Maombi ,hakuna majadiliano" amesema.

London EU Referendum Brexit Symbolbild
Nembo ya BrexitPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Kwa upande wake kansela Angela Merkel ameliambia bunge la shirikisho Bundestag atatumia nguvu zake zote kuepusha Umoja wa Ulaya usivunjike baada ya kura ya Brexit. Akihutubia bungeni kabla ya kuelekea Bruxelles kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya,kansela Angela Merkel amesema anataraji Uingereza itataka kuendeleza uhusiano wa dhati pamoja na Umoja wa ulaya baada ya kutoka,lakini anasisitiza "isitegemee kuwa mambo yatakuwa kama yalivyokuwa"."Anaetaka kuipa kisogo familia hii asitaraji kuwa ataendelea kufaidika bila ya kuwajibika. Kansela Merkel amesisitiza pia "hakuna mazungumzo yatakayoendelezwa pamoja na Uingereza kabla ya kwanza maombi ya kutoka kuwasilishwa."

Wakuu wa benki kuu waahidi kusaidia kukabiliana na kishindo cha Brexit

Katika wakati ambapo Uingereza inajitahidi kutuliza masoko ya hisa juu ya uwezo wake wa kukabiliana na mzozo uliosababishwa na kura ya Brexit mzozo uliopelekea kipimo chake cha kulipa madeni kikipunguzwa kwa alama mbili,viongozi wa benki kuu za nchi za Umoja wa ulaya na dunia wanakutana Sintra nchini Ureno tangu jana kuzungumzia hali ya siku za mbele ya uchumi na sarafu ya kimataifa baada ya Brexit. Katika mkutanio huo utakaomalizika kesho viongozi wa benki kuu za dunia wameonyesha utayarifu wa kusaidia kuimarisha utulivu wa sarafu baada ya Uingereza kuamua kujitoa katika Umoja wa ulaya.

Brüssel Treffen Brexit Jean-Claude Juncker
Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: Reuters/F. Lenoir

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef