1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden: Okoeni demokrasia kwa kumchagua Harris

20 Agosti 2024

Rais wa Marekani Joe Biden alitoa hotuba yake kwa Mkutano Mkuu wa Chama cha Democratic usiku wa kuamkia Jumanne, ambapo alimuunga mkono Kamala Harris amshinde Donald Trump katika uchaguzi wa Novemba 5.

https://p.dw.com/p/4jelN
Wahlkampf in den USA - Joe Biden
Picha: Stephanie Scarbrough/AP Photo/picture alliance

Akizungumza kwa maneno yaliyosikika vyema huku akiwa mwenye nguvu na uchangamfu, Biden aliwataka raia wa Marekani wamchague Harris badala ya Trump, ambaye alimuita mhalifu aliye na mashtaka mahakamani. 

"Huwezi kusema tu kwamba unaipenda nchi yako unaposhinda," alisema Biden, akizungumzia madai ya Trump kwamba matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 ambao alishindwa na Biden, yalichakachuliwa.

Alitoa wito kwa Wamarekani kuhakikisha kwamba nchi yaohaina nafasi ya chuki.

Hakikisho la amani Mashariki ya Kati

Biden aliyebubujikwa na machozi baada ya kualikwa jukwaani na mwanawe wa kike Ashley Biden, alikaribishwa kwa vifijo vilivyodumu kwa dakika nne nzima huku wajumbe katika mkutano huo mkuu, wakiikatisha hotuba yake mara kwa mara kwa maneno "asante Joe."

Israel | Antony Blinken na Isaac Herzog
Waziri wa mambo ya kigeni Marekani Antony Blinken(kushoto) na Rais Isaac Herzog wa IsraelPicha: Kevin Mohatt/AFP/Getty Images

Katika hotuba yake Biden alisema ataendelea na juhudi za kuhakikisha kwamba vita vya Israel dhidi ya Hamas gaza, vinafikia mwisho na amani inapatikana Mashariki ya Kati.

Kiongozi huyo wa Marekani alisema kuwa waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina na wanaotaka kusitishwa vita vya Gaza, "wana hoja."

Biden pia alizungumzia masuala tofauti ambayo yeye pamoja na makamu wake Kamala Harris wameyafanikisha kufikia sasa, ikiwemo ukarabati na kuifanya kuwa ya kisasa miundo mbinu chakavu ya Marekani.

"Tumekuwa na mojawapo ya miaka 4 bora zaidi ya maendeleo."

Aliusifu utawala wake kwa jinsi ulivyoushughulikia uchumi wa Marekani akidai kwamba kwa sasa mishahara inaongezeka huku mfumko wa bei ukizidi kushuka.

Harris kukubali uteuzi Alhamis

Kuwasili kwa Biden katika mkutano huo wa siku nne kunakuja baada ya kushinikizwa kujiondoa kwenye mbio hizo za kuwania urais mwezi uliopita na viongozi wa chama, waliohofia kwamba rais huyo mwenye umri wa miaka 81, ni mzee mno na hatokuwa na nafasi ya kushinda au kuhudumu kwa miaka mingine minne.

Harris ambaye atakubali rasmi uteuzi wake usiku wa Alhamis, aliwasili pasipo kutarajiwa katika mkutano huo huku akishangiliwa pakubwa na wajumbe. Katika ujumbe wake mfupi alioutoa mbele ya wajumbe hao, Harris amemshukuru Rais Biden kwa uongozi wake wa kihistoria na kusema kwamba kwa sasa "wanasonga mbele."

Kamala Harris katika Mkutano Mkuu wa Democratic, Chicago
Kamala Harris katika Mkutano Mkuu wa Democratic, ChicagoPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Harris anaonekana kama anayeleta mwamko mpya katika mkutano huo mkuu wa Democratic kwani kampeni yake imevunja rekodi katika uchangishaji fedha, huku viwanja anakofanyia mikutano yake vikifurika wafuasi wake na kulingana na tafiti za maoni, amefanikiwa pia kukipatia uungwaji mkono chama cha Democratic katika maeneo muhimu yanayodhaniwa kuwa yenye ushindani mkubwa kati ya chama chake na cha mpinzani wake cha Republican.

Mgombea mwenza wa Harris, Gavana maarufu wa jimbo la Minnesota Tim Walz, hapo jana alikutana na kundi la wajumbe katika mkutano huo wa Democratic na wakaimba nyimbo za kuiunga mkono tiketi yake na Harris wakisema, "hawatorudi nyuma."

Hillary Clinton ambaye alihudumu kama waziri wa mambo ya nje katika utawala wa Rais Barack Obama, ameuhutubia mkutano huo pia na akasema kwamba wakati umefika sasa kwa Marekani kupata rais mwanamke.

Lakini Chauncey McLean ambaye ni mkuu wa kamati ya Future Forward, ambayo ni kamati iliyochangisha mamilioni ya dola kumsaidia Harris katika mbio za urais, amewatahadharisha wafuasi wa chama cha Democratic kwamba kura zao bado ni chache kinyume na kinachooneshwa katika tafiti za maoni.

Tafiti hizo ambazo mwezi uliopita zilimuonesha Trump akiwa na uongozi mkubwa dhidi ya Biden, zimeonesha pia kwamba sasa hivi Harris amefanikiwa kupunguza pakubwa pengo hilo, sio tu kitaifa ila pia katika majimbo yenye ushindani kama Pennsylvania ambayo yatakuwa na dhima kubwa katika uchaguzi huo.

Marais wa zamani Obama na Clinton kuhutubia

Jumanne itakuwa zamu ya rais wa zamani Barack Obama kutoa hotuba yake katika mkutano huo mkuu wa chama cha Democratic huku Bill Clinton akiwahutubia wajumbe hao Jumatano.

Kamala Harris und Barack Obama
Rais wa zamani barack Obama akiwa na Kamala HarrisPicha: picture alliance/dpa/AP

Ama kwa upande mwengine nje ya jengo linakofanyika mkutano huo mkuu, kiwingu cha maandamano kimegubika. Waandamanaji ambao hawakufika kwa idadi kubwa kama iliyokuwa imetabiriwa na waandaji wa maandamano hayo, wameuvunja uzio uliokuwa umewekwa na polisi karibu na eneo linakofanyika mkutano huo mkuu. Baadhi ya waandamanaji wamekamatwa kufuatia tukio hilo kisha maafisa wa polisi wakajipanga kwa mstari mrefu kuchukua nafasi ya uzio huo ulioangushwa.

Maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika kupaza sauti zao kupinga vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza. Waliokuwa katika maandamano hayo walikuwa wakiimba nyimbo zinazoitaka Israel isitishe mashambulizi yake Gaza wakidai kwamba ulimwengu mzima unatazama.

Makundi yanayoiunga mkono Palestina yameukosoa utawala wa Rais Joe Biden kwa kuipa msaada Israel.

Chanzo: DW/Reuters/APE