1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Kishida watangaza ushirikiano mpya

11 Aprili 2024

Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida wametangaza mipango ya kuimarisha ushirikiano wa kiusalama baada ya kukutana mjini Washington.

https://p.dw.com/p/4eeta
 Joe Biden akutana na Fumio Kishida mjini Washington
Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida Picha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Mkutano huo wa pande mbili umefanyika wakati Marekani ikitafuta ushirika wenye nguvu zaidi wa Asia, huku China ikiongeza matumizi ya kijeshi na kujiimarisha zaidi katika mizozo ya kikanda katika Bahari ya China Kusini. Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Biden amesema urafiki wao uko imara. 

Biden ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza, Japan, Marekani na Australia zitaunda mtandao wa pamoja wa ulinzi wa makombora ya anga.

QUAD lina hofu ya shughuli za kijeshi katika bahari ya China

Nchi hizo tatu ni wanachama wa muungano wa kundi la mataiafa manne linalofahamika kama Quad, likizijumuisha Marekani, Japan, Australia na India. Kwa upande wake Waziri Mkuu Kishida alisema Marekani na Japan zitaendelea kushughulikia changamoto zinazohusu China kupitia uratibu wa pamoja.

Katika kujibu, China imesema Marekani na Japan zimeichafua na kuishambulia Beijing kuhusu masuala ya Taiwan na bahari ya China Kusini, imeingilia masuala ya ndani ya China na kukiuka kabisa kanuni za msingi zinazosimamia ushirikiano wa kimataifa.