1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Johnson wakutana kwa mkataba mpya

10 Juni 2021

Rais Joe Biden wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson wanakutana mara ya kwanza ana kwa ana kusaka makubaliano mapya, huku suala la Ireland Kaskazini likitanda wingu la shaka baina yao.

https://p.dw.com/p/3ugsb
Großbritannien Vor dem G7-Gipfel in Cornwall - Joe Biden, Präsident der USA
Picha: Joe Giddens/Pool via AP/picture alliance

Biden na Johnson walitazamiwa kukubaliana juu ya muundo mpya wa mkataba uliosainiwa na Winston Churchill na Franklin D. Roosevelt, ambao uliweka malengo ya baada ya Vita vya Pili vya Dunia kwa ajili ya demokrasia, biashara na fursa.

Katika makala iliyochapishwa siku ya Alkhamis (Juni 10), Johnson aliandika kwamba "ulimwengu unahitaji mkutano huu," akisema "muda umefika kuondosha chembe chembe zote za mashaka."

Mkataba huo mpya unajumuisha masuala ya sayansi, teknolojia na biashara, na kutilia mkazo utayarifu wa Marekani na Uingereza kwenye muungano wa kijeshi wa NATO.

Hata hivyo, suala la mahusiano kati ya Uingereza na jimbo lake la Ireland Kaskazini linatajwa kuwa tete.

Biden anaripotiwa kuwaamuru maafisa wake kumbana Johnson juu ya namna anavyolishughulikia suala la Uingereza kujitowa kwenye Umoja wa Ulaya na athari zake kwa mchakato wa amani wa Ireland ya Kaskazini.

Gazeti la Times liliripoti kwamba balozi wa Marekani nchini Uingereza, Yael Lampert, alimuambia waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Brexit, Lord Frost, kwamba "Uingereza inachochea machafuko ya Ireland na Ulaya kutokana na upinzani wake wa ukaguzi katika bandari za jimbo hilo."

Uingereza kuvunja itifaki ya Brexit

Großbritannien Premierminister Boris Johnson
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson.Picha: House of Commons/PA/picture alliance

Awali Uingereza ilikubaliana na Umoja wa Ulaya juu ya itifaki ya ukaguzi wa bidhaa zinazoingia Ireland ya Kaskazini kutoka upande wa bara wa Ufalme wa Uingereza, lakini ikaisitisha baada ya kupingwa na waungaji mkono wa muungano wa Uingereza, wanaosema inabadilisha hadhi ya taifa lao.

Kusitishwa kwa itifaki hiyo kumekuwa sababu ya ghasia mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa Ireland ya Kaskazini kwa muda mrefu.

Johnson alisema Mkataba wa Ijumaa Kuu kwa Ireland Kaskazini ni muhimu kulindwa lakini lazima pia kuwe na ulinzi wa biashara kati ya Uingereza na jimbo lake hilo.

"Kuhusu itifaki ya Ireland Kaskazini, lengo ni kuyadumisha makubaliano ya Belfast ya Ijumaa Kuu, ili kuwe na uwiano kwenye mahusiano ndani ya Ireland Kaskazini. Pia baina ya Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya Ireland biashara iwe huru. Kwa hivyo, tunataka kuhakikisha tuna suluhisho linaloulinda mchakato wa amani, kuuhakikisha, na pia kuuhakikisha uhuru wa kiuchumi na kimipaka kwa Uingereza nzima," alisema Johnson siku moja kabla ya kukutana na Biden.

Akizungumza na kituo cha redio cha Newstalk hivi leo, Waziri Mkuu wa Ireland ya Kaskazini, Micheál Martin, alisema alikuwa anatazamia uingiliaji kati wa Rais Biden kusaidia kuukwamua mkwamo uliopo sasa, kwani aliujuwa msimamo wa Marekani ni kuulinda Mkataba wa Ijumaa Kuu, na aliamini Biden angelihakikisha mshirika wake, Uingereza, anaendelea kuuhishimu.