1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden atarajia mafuta zaidi, kukubaliwa Israel na waarabu

16 Julai 2022

Rais wa Marekani Joe Biden anakutana na viongozi wa Kiarabu nchini Saudi Arabia Jumamosi, akitafuta kuwashawishi washirika wa Ghuba wa Washington kutoa mafuta zaidi na kuijumuisha Israel katika kanda hiyo.

https://p.dw.com/p/4EEIe
Saudi Arabien | US-Präsident Biden trifft Salman bin Abdulaziz
Picha: Bandar Algaloud/Courtesy of Saudi Royal Court/Handout/REUTERS

Biden, katika awamu ya pili ya safari yake ya kwanza ya Mashariki ya Kati kama rais, ameangazia mkutano wa kilele uliopangwa na nchi sita za Ghuba na Misri, Jordan na Iraq huku akipuuza kukutana na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman, hatua ambayo imesababisha ukosoaji nchini Marekani juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Biden alikuwa ameahidi kuitenga Saudi Arabia katika jukwaa la kimataifa kutokana na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi mwaka wa 2018 na maafisa wa Saudia, lakini hatimaye aliamua kwamba maslahi ya Marekani yanataka kurekebiswa, sio mpasuko, katika uhusiano na taifa hilo linaloongoza kwa mauzo aya nje ya mafuta duniani na dola lenye nguvu katika ulimwengu wa Kiarabu.

Biden anahitaji msaada wa Saudia katika wakati huu bei za juu za mafuta ghafi na matatizo mengine yanayohusiana na mzozo wa Urusi na Ukraine na huku akihimiza juhudi za kumaliza vita vya Yemen, ambapo makubaliano ya muda yanaendelea kuheshimiwa. Washington pia inataka kuzuia nguvu ya Iran katika kanda na ushawishi wa China kimataifa.

Saudi Arabien | US-Präsident Biden trifft MSB
Biden na ujumbe wake wakiwa katika mkutano na mrithi wa ufalme wa Saudi, Mohammed bin Salman, katika kasri la kifalme la Al-Salam mjini Jeddah, Julai 15, 2022.Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Rais wa Marekani atafanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi wa Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Iraq kabla ya kushiriki katika mkutano huo mpana zaidi ambapo "ataweka bayana" maono na mkakati wake wa ushiriki wa Marekani katika Mashariki ya Kati, mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani. Jake Sullivan alisema Ijumaa.

"Ana nia ya kuhakikisha kuwa hakuna ombwe katika Mashariki ya Kati kwa Uchina na Urusi kuziba," Sullivan alisema.

Biden atajadili usambazaji wa nishati na wazalishaji wa mafuta wa Ghuba, lakini Washington ilisema haitarajii Saudi Arabia, mwanachama wa nguvu wa OPEC kuongeza uzalishaji mafuta mara moja na atasubiri matokeo ya mkutano wa OPEC+ Agosti 3.

Mataifa ya Ghuba, ambayo yamekataa kuunga mkono nchi za Magharibi dhidi ya Urusi katika mzozo wa Ukraine, kwa upande wake yanatafuta dhamira madhubuti kutoka kwa Marekani juu ya uhusiano wao wa kimkakati ambao umedorora kutokana na kile wanachodhani kuwa kujitoa kwa Marekani kwenye eneo hilo.

Riyadh na Abu Dhabi zimekatishwa tamaa na masharti ya Marekani kuhusu uuzaji wa silaha na kutengwa katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya Marekani na Iran ya kufufua mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 ambayo wanaona yana dosari ya kutoshughulikia masuala ya kikanda kuhusu mpango makombora na mwenendo wa Tehran.

"Takwa muhimu zaidi kutoka kwa uongozi wa Saudi na viongozi wengine wa Ghuba -- na Waarabu kwa ujumla -- ni uwazi wa sera ya Marekani na mwelekeo wake kuelekea kanda," alisema Abdulaziz Sager, mwenyekiti wa Kituo cha Utafiti cha Ghuba chenye makao yake Riyadh.

Saudi Arabien | US-Präsident Biden trifft MSB
Rais Biden akiwa kwenye mkutano na mrithi wa ufalme wa Saudi Mohammed bin Salman mjini Jeddah, Julai 15,2022.Picha: Bandar Algaloud/Courtesy of Saudi Royal Court/Handout/AFP

Ushirika na Israel dhidi ya Iran

Israel, ambayo inashiriki wasiwasi wao juu ya Iran, ilihimiza safari ya Biden katika ufalme huo, ikitumai itaongeza kujongeleana kati ya Saudi Arabia na Israeli kama sehemu ya maelewano mapana ya Waarabu baada ya UAE na Bahrain kuunda uhusiano na Israeli katika makubaliano yaliyoratibiwa na Marekani na kupata baraka za Riyadh.

Katika ishara ya maendeleo chini ya kile Biden alichoelezea kama mchakato wa msingi, Saudi Arabia ilisema Ijumaa itafungua anga yake kwa wabebaji wote wa anga, na kutengeneza njia kwa safari nyingi zaidi za kwenda na kutoka Israeli.

Washington na Riyadh pia zilitangaza kuwaondoa wanajeshi wa Marekani na walinda amani wengine kutoka Tiran -- kisiwa kati ya Saudi na Misri katika eneo la kimkakati kuelekea bandari ya Eilat ya Israel. Wanajeshi hao wamewekwa kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1978 na ambayo yalipelekea makubaliano ya amani kati ya Israel na Misri.

Soma pia: Biden kusitisha mauzo ya silaha UAE na Saudi Arabia

Mkutano wa kilele wa Marekani na viongozi wa Kiarabu utajadili "uratibu na ushirikiano mkali zaidi linapokuja suala la Iran," Sullivan alisema, pamoja na ushirikiano wa kikanda, ikiwa ni pamoja na wa Iraq, ambako Tehran imejenga ushawishi mkubwa. Msaada wa mataifa tajiri ya Ghuba kwa ujenzi wa miundombinu na uwekezaji wa kimataifa pia utajadiliwa.

West Bank | US-Präsident Biden mit Palästinenser- Präsident Abbas
Rais Biden alikutana na rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Bethlehem, aktika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa na Israel, Julai 15, 2022.Picha: EVELYN HOCKSTEIN/REUTERS

Marekani na Israel pia zinataka kuweka msingi wa muungano wa kiusalama na mataifa ya Kiarabu ambao utaunganisha mifumo ya ulinzi wa anga ili kukabiliana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Iran na makombora katika Mashariki ya Kati, duru zimesema.

Soma pia: FBI waweka hadharani uchunguzi wa Septemba 11 kwa amri ya Rais Biden

Mpango kama huo utakuwa mgumu sana kwa mataifa ya Kiarabu ambayo hayana uhusiano na Israel na yanapinga kuwa sehemu ya muungano unaoonekana kuwa dhidi ya Iran, ambayo imejenga mtandao mkubwa wa mawakala kuzunguka eneo hilo ikiwa ni pamoja na Iraq, Lebanon na Yemen.

Afisa mkuu wa Imarati Anwar Gargash alisema siku ya Ijumaa wazo la kile kinachoitwa NATO ya Mashariki ya Kati ni gumu na kwamba ushirikiano wa pande mbili ni wa haraka na wenye ufanisi zaidi.

UAE, alisema, haitaunga mkono mkakati wa makabiliano: "Tuko wazi kwa ushirikiano, lakini sio ushirikiano unaolenga nchi nyingine yoyote katika eneo hili na ninaitaja makhsusi Iran."