1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden asema mashambulizi ya Israel yanapasa kusitishwa

9 Februari 2024

Rais Joe Biden wa Marekani amesema kampeni ya jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza kujibu mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyofanywa na Hamas imepitiliza na inapaswa kusitishwa.

https://p.dw.com/p/4cDMG
Rais Joe Biden wa Marekani
Rais Joe Biden wa Marekani asema ulipizaji kisasi wa Israel katika Ukanda wa Gaza umepitiliza.Picha: picture alliance / CNP/AdMedia

Rais huyo wa Marekani alisema kwamba watu wasio hatia wamekuwa wakipoteza maisha kwenye operesheni hiyo ya Israel.

"Nina mtazamo kama mnavyojua, kwamba uendeshaji wa operesheni ya majibu umepitiliza. Kuna watu wengi wasio na hatia wanaokufa kwa njaa, watu wengi wasio na hatia ambao wako katika shida na kufa. Na haina budi kusimama." Alisema.

Soma zaidi: Blinken aondoka Mashariki ya Kati bila mafanikio

Hatua ya Marekani kuunga mkono vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas imesababisha mkururo wa mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani katika kanda ya Mashariki ya Kati, pamoja na ukosoaji dhidi ya utawala wa Biden kutoka ndani na nje ya nchi hiyo. 

Miezi kadhaa ya mashambulizi na mzingiro wa Israel vimezidisha mzozo wa kiutu kote Gaza.

Lakini Rais huyo mwenye umri wa miaka 81 alisema ameshinikiza kuruhusu uingizaji wa misaada ya kibinaadamu katika eneo hilo.