1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kuitisha mkutano wa kilele kati ya Afrika na Marekani

Daniel Gakuba
19 Novemba 2021

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema rais wa nchi hiyo Joe Biden ataandaa mkutano wa kilele na viongozi wa Afrika, kwa azma ya kuimarisha ushirikiano kati ya Marekani na Afrika.

https://p.dw.com/p/43Dzd
Strategischer Dialog zwischen USA und Ukraine
Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa MarekaniPicha: Leah Millis/AP/Reuters/dpa/picture alliance

Hayo Antony Blinken ameyatangaza leo mjini Abuja, ambako anaendelea na ziara yake ya mataifa kadhaa ya Afrika.

''Kama ishara ya dhamira yetu ya dhati kwa ushirikiano na bara la Afrika, Rais Biden anaazimia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele na viongozi wa Afrika, katika juhudi za hali ya juu za kidiplomasia za kuuimarisha na kuuboresha uhusiano wetu kadri iwezekanavyo,'' amesema waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani.

Soma zaidi: Blinken akutana na viongozi Kenya

Hata hivyo, Blinken ambaye hii ni ziara yake ya kwanza Afrika kama waziri wa mambo ya nje wa Marekani, hakusema chochote kuhusu tarehe ya mkutano huo.

Mbio za mataifa makubwa kuwania ushawishi

Azma hiyo ya Rais Biden inatangazwa wakati China ikiendeleza mkakati wa mikutano ya mara kwa mara na viongozi wa Afrika, mmojawapo wa mikutano hiyo ukitarajiwa kufanyika mwezi huu nchini Senegal, ambako ni kituo cha mwisho cha ziara hii ya Blinken.

Ufaransa, Uingereza na Japan huwa pia zinaandaa mikutano ya kilele na viongozi wa Afrika.

Muhammadu Buhari, Präsident von Nigeria
Rais wa Nigeria, Muhammadu BuhariPicha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Baada ya kuwasili Nigeria hapo jana, waziri Blinken alifanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Muhammadu Buhari, ambayo yalijikita katika masuala ya usalama wa Nigeria na ukanda wa Afrika Magharibi, pamoja na demokrasia inayosuasua katika ukanda huo.

Haki za binadamu Nigeria zapigwa kurunzi

Siku chache kabla ya mwanadiplomasia mkuu huyo wa Marekani kuwasili Nigeria, taarifa zilizovuja zilieleza kuwa wanajeshi wa Nigeria waliwafyatulia risasi watu waliokuwa wakiandamana kwa amani kwenye kituo cha ushuru mjini Lagos Oktoba mwaka jana, kisa kilicholinganishwa na mauaji ya kiholela.

Soma zaidi: Blinken aonya kuhusu haki za binaadamu, India

Blinken aliligusia suala hilo katika mkutano wa pamoja na mwenzake wa Nigeria, Geoffrey Onyeamay, na akasema kulingana na uchunguzi wa ripoti hiyo utakavyohitimishwa, wahusika katika uhalifu huo dhidi ya ubinadamu watapaswa kuadhibiwa, kupitia mchakato ulio wazi kabisa.

Äthiopien Symbolbild Tigray-Konflikt
Ziara ya waziri Blinken Afrika inafanyika wakati bara hilo lilikabiliwa na mizozo lukukiPicha: Eduardo Soteras/AFP

Akiuzungumzia kisa hicho kwa mara ya kwanza hadharani, Rais Buhari alimwambia Blinken kuwa utawala wake utafuata hatua zitakazochukuliwa na serikali ya jimbo ambayo iliagiza uchunguzi huo.

Apigia debe demokrasia na uhuru wa kiraia

Ziara ya waziri Blinken ya nchi tatu za Afrika ilianzia nchini Kenya, ambako alisisitiza ulazima wa kusitisha mapigano bila masharti katika mzozo wa kivita nchini Ethiopia, na kuhimiza kurejeshwa kwa uongozi wa kiraia nchini Sudan.

Ziara yake barani Afrika imekuja wakati nchi kadhaa za bara hilo zikighubikwa ni mizozo. Katika hotuba zake ametilia mkazo umuhimu wa raia kukusanyika kwa amani bila vizuizi, na kueleza maoni yao kwa uhuru.

 

afpe, rtre