1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin. Misaada yamiminika kusini mwa Asia.

10 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CETL

Mataifa mbali mbali duniani yanapeleka makundi ya waokoaji na wa kutoa misaada kusini ya bara la Asia kusaidia katika kazi ya uokoaji baada ya tetemeko kubwa la ardhi. Ujerumani imetoa msaada wa Euro 55,000 za msaada wa dharura na inatuma kundi la watu 15 watakaosaidia katika kuwatafuta watu walionusurika katika maafa hayo.

Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 3 kwa ajili ya huduma za kiafya pamoja na madawa. Japan, Uingereza na Uturuki pamoja na Umoja wa falme za Kiarabu UAE, ni miongoni mwa nchi zilizopeleka misaada ya mwanzo.

Rais wa Marekani George W. Bush pia anatuma helikopta za kijeshi, msaada ambao Pakistan imekuwa hapo kabla ikisita kuukubali.

Wakati huo huo , umoja wa mataifa umetenga maeneo matatu ya kutoa misaada ya dharura nchini Pakistan ili kuratibu juhudi za kimataifa za utoaji wa miasaada katika kile maafisa wa Pakistan wanachokiita maafa makubwa kabisa kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo.

Na huko Amerika ya kati, mamia ya watu wamekufa katika maporomiko ya matope na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Stan kilicholikumba eneo hilo wiki iliyopita.

Eneo lililoathirika zaidi ni Guatemala, ambako zaidi ya wahanga 1,400 wameuwawa wakati maporomoko makubwa kabisa yalipokizoa kijiji cha Panabaj.

Kimbunga Stan pia kimeharibu maeneo ya Mexico na El Salvador, kikiwaacha mamia kwa maelfu ya watu wakiwa hawana makaazi.

Juhudi za uokozi zinaendelea kuweza kuwafikia watu wanaoishi katika maeneo ya mbali kwa kuwapelekea maji , chakula na madawa.