1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Iran kutoachiliwa kuidhuru Umoja wa Mataifa

6 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDEn

Ujerumani imesema Iran haiwezi kuachiliwa kuidhuru Umoja wa Mataifa kwa kuendelea na mpango wake wa nuklea.

Kauli hiyo ya Kansela Angela Merkel ni miongoni mwa kauli kali kabisa kutoka kwa viongozi wa Ulaya tokea Iran ilipokataa madai ya Umoja wa Mataifa kutaka isitishe urutubishaji wa uranium ili nayo badala yake iweze kupatiwa vifuta jasho vya kiuchumi na kisiasa.

Merkel ametowa kauli yake hiyo leo katika hotuba kwa wabunge.

Hata hivyo Merkel ameweka wazi kwamba hakuna uamuzi wa kuchukuliwa kwa hatua ya kijeshi dhidi ya Iran.

Maafisa wa serikali ya Ujerumani wameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba Merkel alikuwa akisita sita kujiunga na shinikizo la kuwekewa vikwazo kwa nchi hiyo lakini hatimae ameanza kupoteza matumaini kwamba mazungumzo yanaweza kufanikiwa na nchi ambayo rais wake ametowa wito hadharani wa kutaka kuangamizwa kwa taifa la Israel.

Wakati huo huo mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Umoja wa Ulaya na Iran juu ya mzozo huo wa nuklea ambayo yalikuwa yaanze leo hii yameahirishwa na yumkini yakafanyika hapo Ijumaa.