Benjamin kuzungumzia sera yake kuu ya nje
5 Machi 2018Viongozi hao wawili Benjamin Netanyahu wa Israel na Donald Trump wa Marekani wanatarajiwa kuwa na msimamo wa pamoja dhidi ya uchokozi unaofanywa na Iran hasa nchini Syria na kutoa wito wa kuboreshwa kwa mpango uliyoafikiwa wa Nyuklia kati ya taifa hilo na mataifa sita yaliyo na nguvu duniani. Trump ametishia kuyavunja makubaliano hayo.
Katika mkutano wao utakaofanyika kwenye ikulu ya White house, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anatarajiwa kumpongeza Trump kwa hatua yake ya kuitambua Jerusalem kama mji Mkuu wa Israel na kuhamisha ubalozi wa Marekani katika eneo hilo.
"Natarajia kuzungumza naye kuhusu masuala mengi lakini kwanza ni juu ya Iran, uchokozi wake, matarajio yake ya nyuklia na hatua yake pia ya kichokozi katika eneo la Mashariki ya kati na mipaka yetu. Nadhani hatua ya kuzuwia uchokozi huu ni lengo letu la pamoja na la mataifa mengine katika eneo,”alisema Benjamin Netanyahu.
Hata hivyo ziara hii ya Nentanyahu nchini Marekani inakuja wakati ambapo waziri mkuu huyo anapitia wakati mgumu nyumbani, wakati Mwanasheria Mkuu akifikiria iwapo achukue hatua kutokana na mapendekezo ya polisi kwamba amfungulie mashtaka dhidi ya rushwa na mashitaka mengine.
Netanyahu na mkewe Sara, waliwasili mjini Washington hapo jana siku mbili baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa na polisi nchini Israel juu ya tuhuma za rushwa zinazofungamanishwa na kampuni ya simu ya telecom.
Mkutano wake na Trump na hotuba yake aliyoitoa katika mkutano wa kamati ya masuala ya Umma ya Marekani ambayo ina jukumu la kulinda maslahi ya Israel (AIPAC) inammpa nafasi Netanyahu kuangazia wasiwasi katika sera yake ya kigeni pamoja na mafanikio.
Kikubwa katika orodha yake hii ni Marekani kuutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, hatua ambayo iliwakasirisha wapalestina na kukosolewa Kimataifa lakini hilo limempa sifa Netanyahu nchini Israel. Awali rais wa Guatemala Jimmy
Morales alitangaza mipango ya nchi yake ya kuuhamisha ubalozi wake mjini Jerusalem.
Aidha Mchakato wa mazungumzo ya amani au upatanishi kati ya Israel na palestina umesimama tangu rais Trump kutangaza hatua hiyo ya kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel lakini maafisa wa Ikulu ya Marekani wanasisitiza kwamba watawasilisha mpango wa amani hivi karibuni.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa
Mhariri: Yusuf Saumu