1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Vikwazo vya silaha dhidi ya Uchina viondoshwe

2 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFQw

Rais Jacques Chirac wa Ufaransa amekariri kuwa anaunga mkono hatua ya kuondosha vikwazo vya biashara ya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Uchina zaidi ya miaka kumi ya nyuma.Kwa mujibu wa Shirika la habari la Uchina XINHUA,rais Chirac alipozungumza kwa simu na Rais Hu Jintao wa Uchina alimuhakikishia kuwa vikwazo hivyo vimepitwa na wakati na vinapaswa kuondoshwa. Amesema hatua hiyo itasaidia kuendeleza uhusiano kati ya Uchina na Umoja wa Ulaya.Uchina iliwekewa vikwazo vya silaha,baada ya serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua kali na kusababisha mmuagiko wa damu mwaka 1989 wakati wa maandamano ya kuunga mkono demokrasia.Mwaka jana Umoja wa Ulaya ulikubali kuviondosha vikwazo hivyo mwishoni mwa mwezi wa Juni mwaka 2005.Mpango huo lakini umekosolewa na nchi nyingi ikiwa ni pamoja na Uingereza na Marekani,hasa kwa sababu ya mivutano inayozidi kushika kasi kuhusu suala la Taiwan. Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani sawa na rais Chirac ametoa muito wa kuviondosha vikwazo hivyo,ingawa serikali ya muungano wa chama chake cha SPD na cha Kijani haikubaliani kuhusu suala hilo.