Bayern yaonywa kujipiga kifua, msimu bado mbichi
28 Septemba 2012Bayern wameshinda mechi zao zote tano za mwanzo msimu huu katika ligi ya bundesliga na wana tofauti ya pointi nane mbele ya mahasimu wao ambao ni mabingwa watetezi Borussia Dortmund. Rummenige amesema ataukanyaga mguu chini na hataanza kujivunia.
Hali ilikuwa kama hiyo msimu uliopita baada ya mechi sita, tofauti baina ya timu hizo mbili ilikuwa point inane kabla ya Dortmund kurejea kwa kishindo na kutetea taji lake. Rummenige anasema lengo lao kuu ni kutwaa taji la BUNDESLIGA.
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Löw, ameelezea furaha yake kufuatua kurejea katika hali nzuri na kupona jeraha kiungo Bastian Schwiensteiger kabla ya ratiba ya mwezi ujao ya mechi za kufuzu katika dimba la dunia.
Ujerumani itasafiri hadi Dublin kupambana na Jamhuri ya Ireland mnamo Oktoba 12 na kisha kuwaalika Sweden siku nne baadaye mjini Berlin katika mchuano wa kundi C kwa mechi za kufuzu kwa kombe la dunia 2014 nchini Brazil. Kiungo huyo wa Bayern Munich Schweinsteiger, mwenye umri wa mika 28, hajaichezea nchi yake tangu mchuano wa nusu fainali wa dimba la UEFA EURO 2012 ambapo walishindwa na Itali mjini Warsaw mwezi Juni.
Kisha akakosa mechi ya kirafiki waliyoshindwa magoli matatu kwa moja na Argentina nyumbani na mechi za mwanzo za kufuzu kwa kombe la dunia ambazo walishinda zote dhidi ya Visiwa vya Faroe na Austria.
Lakini, hata hivyo, amekuwa na mwanzo mzuri na Bayern msimu huu, ikiwa ni pamoja na kufunga magoli mattau na moja katika ushindi wao wa mbili wka moja dhidi ya Valencia katika mchuano wa kombe la Ligi ya Mabingwa.
Löw ambaye pia amemsifu Lucas Podolski kwa mwanzo wake mzuri wa maisha yake mapya katika klabu ya Arsenal na akamuunga mkono beki anayekabiliwa na shinikizo wa Borussia Dortmund Marcel Schmelzer, atakitaja kikosi chake mnamo Oktoba tano.
Tennis
Bingwa wa sasa wa mataji ya Wembledon na US Open, Serena Williams, amejiondoa kutoka mashindano ya China Open kwa sababu ya homa, huku dakake Venus pia akijiondoa akitaja sababu ya jeraha la mgongo.
Serena ambaye alidhihirisha umahiri wake katika mchezo wa Tennis mwaka huu kwa kupandisha idadi ya mataji yake makuu ya Grand Slam kufika 15 na kushinda dhahabu katika michezo ya Olimpiki, alijiondoa katika kinyang'anyiro hicho siku mbili kabla ya kuanza kwa duru ya kwanza.
Hilo ni pigo kubwa kwa waandalizi wa dimba hilo la Beijing kwa sababu mwana Tennis huyo anayeorodheshwa nambari nne ulimwenguni, na ambaye tayari amefuzu kwa vinyang'anyiro vya kumalizia msimu vya Ubingwa wa WTA mjini Istanbul, Uturuki mwezi ujao, ni mmoja wa wachezaji bora zaidi wa dimba hilo.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters
Mhariri: Miraji Othman