1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern hatimaye wavunja benki kwa ajili ya Kane

10 Agosti 2023

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich wanaripotiwa kufikia makubaliano Alhamis na Tottenham Hotspur kwa ajili ya uhamisho wa nahodha wa timu ya taifa ya England Harry Kane. Haya ni kulingana na tovuti ya Atheltic.

https://p.dw.com/p/4Uzt9
Kandanda - Kombe la Dunia Qatar 2022 I England vs Iran
Nahodha wa England Harry KanePicha: Javier Garcia/Shutterstock/IMAGO

Bayern ambao hawajatoa tamko kuhusiana na ripoti hiyo, wamejaribu kwa miezi sasa kumnunua mshambuliaji huyo huku ripoti zikiarifu kwamba dau watakalowalipa Spurs litakuwa yuro milioni 100. Iwapo Kane atajiunga na Bayern, huo utakuwa ni uhamisho ghali zaidi wa mchezaji katika historia ya Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga.

The Bavarians kama wanavyojulikana Bayern kwa jina la utani naambao walilishinda taji la Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, kwa mara ya 11 mfululizo msimu uliopita, wamekuwa wakimtaka sana Kane kwa ajili ya kuinoa tena safu yao ya mashambulizi na kupigania taji la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, Champions League kwa mara nyengine tena.

Tovuti ya Athletic inasema mpira sasa upo kwa Kane mwenyewe kuamua iwapo anataka kujiunga na miamba hao wa Ujerumani. Kane amesalia na mwaka mmoja tu katika kandarasi yake na Tottenham Hotspur.

Bayern wanauanza msimu wao Jumamosi watakapocheza mechi ya Super Cup dhidi ya RB Leipzig. Wiki moja baadae, Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga, itakuwa inaanza msimu wake mpya.

Chanzo: Reuters