1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lataka siku 90 za kusitishwa mapigano

29 Aprili 2020

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapanga kutoa wito wa usitishwaji mapigano kwa kipindi cha siku 90 duniani kote, ikiwa ni sehemu ya vita dhidi ya janga la COVID-19.

https://p.dw.com/p/3bYLv
New York UN Sicherheitsrat Russland Veto MH17
Picha: picture-alliance/dpa/J. Szenes

Katika rasimu ya awali iliyoandikwa kwa pamoja kati ya Ufaransa na Tunisia, pendekezo lilikuwa ni usitishaji wa mapigano kwa siku 30, sambamba na kutoa wito wa kukomesha uhasama kwenye mataifa yenye mizozo na kuongeza ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na virusi vya korona.

Lakini rasimu mpya iliyopitiwa juzi Jumatatu na nakala yake kuonekana jana Jumanne na shirika la habari la AFP, inataka pande husika katika mizozo inayotumia silaha kuanza mara moja kile kinachoitwa "kipindi cha mapumziko kwa ajili ya ubinaadamu" kwa angalau siku 90 mfululizo.

Usitishwaji huo ni kwa ajili ya kuwezesha ufikishwaji wa misaada ya kibinaadamu kwa watu walioko kwenye maeneo ya kivita, kwa mujibu wa rasimu hiyo. 

Hadi sasa, hakuna tarehe iliyowekwa kwa ajili ya kupigiwa kura azimio hilo, kwani suala tete zaidi, ambalo ni dhima ya Shirika la Afya Duniani, WHO, ambalo linakosolewa vikali na Marekani, halijatatuliwa.

Mnamo tarehe 23 Machi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano kote ulimwenguni, ili kutoa nafasi kwa mataifa kukabiliana na janga la COVID-19.

Hata hivyo, rasimu ya azimio hili la sasa inahusisha tu mataifa ambayo tayari migogoro yake inafuatiliwa na Baraza la Usalama, ikiwemo ya Syria, Yemen, Afghanistan, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya, Colombia na Sudan.

Baraza la Usalama lashindwa kuzungumzia Venezuela

Präsident von Venezuela - Nicolas Maduro
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ambaye nchi yake inakabiliwa na mzozo wa muda mrefu wa kiuchumi na kisiasa.Picha: picture-alliance/dpa/Prensa Miraflores/J. Zerpa

Katika hatua nyengine, kikao cha ndani cha Baraza hilo la Usalama hapo jana kilishindwa kutoa kauli yoyote juu ya hali inavyoendelea nchini Venezuela, huku wajumbe wa Umoja wa Ulaya wakisema janga la virusi vya korona linatishia usalama wa raia wa taifa hilo la Amerika Kusini, ambalo tayari linakabiliwa na hali mbaya sana ya kiuchumi, kijamii na kibinaadamu.

Tamko la pamoja kati ya Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Estonia na Poland lilielezea wasiwasi wa Umoja wa Ulaya jinsi hali inavyozidi kuwa mbaya nchini Venezuela.

Umoja wa Ulaya ni mfadhili mkubwa kwenye kuutatuwa mzozo wa kibinaadamu unaowakabili raia wa Venezuela ukiwa unatoa zaidi ya nusu ya fedha zinazohitajika, lakini kwa pamoja mataifa hayo yalitaka juhudi za haraka zichukuliwe kuinusuru hali ya mambo.

Wanachama hao wa Umoja wa Ulaya waliunga mkono wito wa Guterres, aliyetaka pawepo na ushirikiano baina ya mifumo ya Umoja wa Mataifa, shirika la Msalaba Mwekundu na mashirika mengine ya kimataifa na yasiyo ya kiserikali ili kuwezesha utolewaji msaada wa kibinaadamu.