1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama laitisha kikao cha dharura kujadili Rafah

28 Mei 2024

Israel inaendelea kukumbwa na wimbi la shutuma kutoka jumuiya ya kimataifa kuhusiana na shambulizi lake ambalo maafisa wa Gaza wamesema liliwauwa watu 45. Baraza la Usalama limeitisha kikao cha dharura.

https://p.dw.com/p/4gM4C
Shambulizi Rafah
Maafisa wa afya wa Gaza walisema watu 45 waliuawa katika shambulizi la angani la Israel katika kambi ya wakimbiziPicha: Jehad Alshrafi/dpa/picture alliance

Shambulizi hilo lilisababisha moto mkubwa katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina. Israel kupitia waziri mkuu Benjamin Netanyahu imesema inachunguza tukio hilo ililoliita"ajali ya kusikitisha" na athari zake kwa raia.

Jeshi la Israel lilisema shambulizi hilo la Jumapili usiku kusini mwa Rafah liliwalenga na kuwauwa maafisa wawili waandamizi wa Hamas lakini pia likasababisha moto ambao Wapalestina na nchi nyingi za Kiarabu zimelaani kwa kuliita tukio hilo "mauaji ya kikatili". Msemaji wa Baraza la Usalama wa Kitaifa la Marekani amesema Israel lazima ichukue tahadhari zote kuwalinda raia. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati Tor Wennesland ameitaka Israel kufanya uchunguzi wa kina na wa wazi kuhusu tukio hilo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao cha dharura kujadili shambulizi la RafahPicha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Jeshi la Israel limesema limeanzisha uchunguzi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulizi hilo akisema liliwalenga raia wasio na hatia ambao walikuwa wametafuta hifadhi kutokana na vita vinavyoendelea. Amesema "hakuna mahali salama katika Ukanda wa Gaza. Ukatili huo lazima ukomeshwe." Baraza la Usalama limeitisha kikao cha dharura kujadili shambulizi la Rafah. 

Umoja wa Ulaya kujadili haki za binaadamu la Israel

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kufanya mkutano wa Baraza la Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na Israel ili kutathmini uzingatiaji wa Israel wa makubaliano ya jumuiya hiyo ya wajibu wa haki za binaadamu.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell ametangaza hatua hiyo mjini Brussels wakati akiongeza shinikizo dhidi ya Israel kutii uamuzi kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Haki – ICJ wa kusitisha mashambulizi yake katika mji wa Rafah, kusini mwa Gaza.

Moto katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina Rafah
Israel ilisema shambulizi la angani katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina lilikuwa ni "kosa kubwa."Picha: REUTERS

Borell amesema inakwenda kinyume na uamuzi wa ICJ, kwa kuongeza shughuli zake za kijeshi, mashambulizi ya mabomu na kuongeza idadi ya raia wanaouawa na kujeruhiwa. Mkuu huyo wa sera za kigeni amesema mawaziri wa mambo ya kigeni wamemtaka apendekeze hatua nyingine zaidi kuhakikisha Israel inatii uamuzi wa ICJ.

Umoja wa Ulaya umeendelea kulaani mashambulizi ya kigaidi ya Hamas ya Oktoba 7 nchini Israel ambayo yaliwauwa zaidi ya watu 1,200 na watu 250 kuchukuliwa mateka lakini ukosoaji wa namna Israel inavyoshambulia Gaza umekuwa ukiongezeka.

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya pia walifanya mazungumzo yasiyo rasmi na mawaziri wenzao kutoka Saudi Arabia, Jordan, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar, Pamoja na katibu mkuu wa Mataifa ya Jumuiya ya Kiarabu.

Baada ya mkutano huo, Borell alisema mawaziri kutoka mataifa ya Kiarabu yalipendekeza kufanyika kongamano la kimataifa la kutekelezwa kwa suluhisho la mataifa mawili kwa mgogoro wa Israel na Hamas.

dpa