1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Baraza kuu la UN latarajiwa kupiga kura kuhusu mzozo wa Gaza

12 Desemba 2023

Baraza Kuu la UN linaonekana kuwa tayari kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano ili kuwezesha kupelekwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza baada ya Marekani kupinga hatua hiyo katika Baraza la Usalama

https://p.dw.com/p/4a4ye
Matokeo ya kura yanaoneshwa baada ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa kupigia kura usitishwaji vita katika ukanda wa Gaza ili kupelekwa kwa msaada wa kibinadamu
Matokeo ya kura yanaoneshwa baada ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa kupigia kura usitishwaji vita katika ukanda wa GazaPicha: Bebeto Matthews/AP Photo/picture alliance

Kura hiyo inafanyika siku moja baada ya wajumbe 12 wa baraza la usalama kufanya ziara katika mpaka wa Rafah kwenye upande wa Misri, eneo la pekee ambalo misaada kidogo ya kibinadamu na mafuta imevukishwa kuingia Gaza. Marekani haikutuma muakilishi wake katika ziara hiyo. Richard Gowan, mkurugenzi katika shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia migogoro ya kimataifa, amesema, katika kila hatua, Marekani inaonekana kujitenga na msimamo wa Umoja wa Mataifa.

Marekani na Israel zinapinga usitishaji wa vita

Marekani na Israel zinapinga usitishaji wa vita kwa sababu kulingana na mataifa hayo, hatua hiyo italinufaisha kundi la Hamas pekee. Marekani inaunga mkono kusimamishwa kwa muda kwa mapigano ili kuwalinda raia na kuruhusu kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas baada ya mashambulizi ya kushtukiza ya Oktoba 7 yaliyofanywa na kundi la Hamas nchini Israeli. Baadhi ya wanadiplomasia na waangalizi, wanatabiri kuwa kura ya leo itapata uungwaji mkono mkubwa huku kura thuluthi mbili zikihitajika.

Nchi za Kiarabu zapinga kupeleka wanajeshi wao katika ukanda wa Gaza

Katika Kongamano la kila mwaka la Doha lililomalizika jana Jumatatu, Qatar ilisisitiza kwamba hakuna nchi ya Kiarabu itakayopeleka vikosi vyake kulinda amani baada ya kukamilika kwa vita katika ukanda wa Gaza.

Moshi unapaa kufuatia shambulizi la Israel katika ukanda wa Gazamnamo Desemba 11, 2023
Moshi unapaa kufuatia shambulizi la Israel katika ukanda wa GazaPicha: Clodagh Kilcoyne/REUTERS

Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed Bin Abdulrahman al-Thani, amesema hakuna yeyote kutoka kanda hiyo atakayekubali kuingilia kati baada ya vita hivyo kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas na pia amepinga kupelekwa kwa vikosi vya kimataifa katika ukanda huo kutokana na hali ilivyo kwa sasa.

Soma pia; Israel inaweza kulitokomeza kabisa kundi la HamasI

Suala la Palestina ni nyeti mno kwa viongozi wa mataifa ya kiarabu, ambapo vita hivyo vimesababisha maandamano makubwa katika nchi kadhaa.

Katika hatua nyingine, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNWRA) Philippe Lazzarini amesema leo mwishoni mwa ziara yake ya usiku kucha katika Ukanda wa Gaza kwamba raia katika eneo hilo wanavumilia kile alichokiita "kuzimu duniani" wakati vita vya Israel dhidi ya Hamas vikiendelea.

Soma pia:Baraza la Usalama kukutana na waathirika wa vita vya Gaza

Katika ujumbe alioutuma kupitia mtandao wa X ambao awali ulijulikana kama twitter, Lazzarini amesema kuwa katika ukanda wa Gaza, msaada unaohitajika ni mkubwa na kwamba shirika lake linapitia kile alichokiita ''Hali isiyowezekana''