1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Bangladesh: Waziri Mkuu Sheikh Hasina ajichimbia madarakani

10 Januari 2024

Waziri mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina ameshinda muhula mwingine madarakani kufuatia uchaguzi mkuu wenye utata uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani na kuitikiwa na wapigakura wachache sana.

https://p.dw.com/p/4b5HO
Bangladesch | Sheikh Hasina, waziri mkuu wa Bangladesh
Hasina alisema Jumatatu kwamba maendeleo ya kiuchumi yalikuwa kipaumbele chake katika miaka mitano ijayoPicha: Mohammad Ponir Hossain/REUTERS

Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina amepata muhula wa nne mfululizo madarakani siku ya Jumatatu huku chama chake cha Awami League kikichukua robo tatu ya viti bungeni kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata.

Kura hiyo ilisusiwa na chama kikuu cha upinzani cha Bangladesh Nationalist Party (BNP), ambao waliuelezea kuwa "haramu." BNP ilitaka kuundwe serikali ya muda isiyoegemea upande wowote kusimamia uchaguzi, ikisema kuwa serikali ya Hasina haiwezi kufanya uchaguzi huru na wa haki. Lakini chama tawala kilikataa wito huo.

Tume ya uchaguzi ilisema siku ya Jumatatu kwamba chama wa Awami League kilishinda viti 222 kati ya 298 vya ubunge katika uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumapili. Mamlaka zilisitisha uchaguzi katika majimbo mawili, moja kwa sababu ya vurugu wakati wa uchaguzi, na lingine kuhusiana na kifo cha mgombea huru kutokana na sababu za kiasili wiki moja kabla.

Wakosoaji wanasema udhibiti wa Hasina wa bunge ni mkubwa hata zaidi ya zinavyoonesha takwimu za viti 222, kwa sababu vyama vingi vidogo vya upinzani na wagombea huru wanashirikiana na chama tawala. Jasmin Lorch, mtafiti mwandamizi kutoka taasisi ya Ujerumani ya Maendeleo ya Uendelevu, IDOS, aliutaja kuwa "uchaguzi wa kiimla."

"Hakukuwa na chama cha kweli cha upinzani katika kinyanganyiro cha uchaguzi, na serikali ya chama cha Awali league ilifhibiti kikamilifu mchakato wa uchaguzi," alisema.

Bangladesh | Kupaishwa kwa Sheikh Hasina
Waziri Mkuu Sheikh Hasina pamoja na wabunge wengine wakila kiapo kama wabunge, Jumatano kufuatia uchaguzi wa Januari 7.Picha: Press Information Department of Bangladesh

"Kiujumla, huu ulikuwa uchaguzi wa kiimla, ambao ulilenga kuimairsha mamlaka ya chama tawala na kuunda mfano wa demokrasia, katika kile ambacho kiukweli ni utawala wa siasa za kiimla."

Nini kilisababisha uitikiaji mdogo wa wapigakura?

Wabangladesh walijiweka mbali kwa kiasi kikubwa na uchaguzi huo, uliokumbwa na vurugu za kisiasa na ukosoaji wa kimataifa. Ushiriki ulikuwa katika asilimia 41.8, kulingana na tume ya uchaguzi, ikilinganishwa na zaidi ya asilimia 80 katika uchaguzi uliyopita wa mwaka 2018.

Baadhi wanasema ushiriki wa wapigakura ulikuwa mdogo hata zaidi. Wakati maripota wa DW walipotembelea vituo vya kupigia kura katika mji mkuu Dhakar, katika saa ya mwisho ya kupiga kura siku ya Jumapili, walivikuta vikiwa vitupu kwa sehemu kubwa. Maafisa wake wasimamizi walisema uitikiaji wa wapigakura kwenye vituo hivyo ulikuwa karibu asilimia 20.

Soma pia: Upinzani Bangladesh waitisha mgomo nchi nzima kesho Jumapili

Uitikiaji ulikuwa mdogo pia katika vituo vingine ilivyotembelea DW siku nzima ya uchaguzi, isipokuwa tu kituo kimoja cha kiunga cha Mirpur. "Idadi ndogo ya waliojitokeza kwenye uchaguzi inaonyesha kuwa raia wengi wa Bangladesh hawakuzingatia mchakato huo kuwa halali na hawakuuona kama njia ya maana ya kuelezea matakwa yao ya kisiasa," Lorch alisema.

Huu ni uchaguzi mkuu wa tatu nchini Bangladesh katika kipindi cha miaka 15 iliyopita ambao ulitiwa doa na wasiwasi wa kuaminika. Kura mbili za awali - zilizofanyika 2018 na 2014, mtawalia - pia zilionekana kuwa na dosari. Zilikumbwa na ghasia na madai mengi ya wizi wa kura, ambayo mamlaka ilikanusha. Chama cha BNP kilishiriki katika kura ya 2018 lakini kilisusia uchaguzi wa 2014.

Wasiwasi kuhusu demokrasia na haki za binadamu

Katika maandalizi ya kura hiyo, viongozi wa Bangladesh walishutumiwa kwa kuwabana wapinzani kwa kutumia mashtaka ya uwongo kufuatia maandamano mabaya ya kuipinga serikali mwishoni mwa Oktoba. BNP ilisema polisi waliwazuwilia karibu wanaharakati wake 25,000 na kwamba wengi zaidi wako mafichoni.

Bangladesh | Maandamano ya nchi nzima
Wafuasi wa upinzani wamekuwa wakidandamana kupinga utawala wa chama cha Wami League, na kusababisha uharibifu wa mali na miundombinu.Picha: Mamunur Rashid/NurPhoto/picture alliance

Kiongozi wa BNP mwenye umri wa miaka 78 Khaleda Zia amekuwa akiishi chini ya kifungo cha nyumbani, na maafisa wengine wengi waandamizi wa chama pia wako jela au uhamishoni. Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, makundi ya haki za binadamu na wakosoaji wameilaumu mara kwa mara serikali ya Hasina kwa kukandamiza upinzani, kuzuia uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari, na kutenda ukiukaji wa haki za binadamu.

Na baada ya matokeo ya karibuni zaidi ya uchaguzi, Sultan Mohammed Zakaria, mtaalam wa Bangladesh katika shirika la haki za binadamu la Amnesty International nchini Marekani, anahofia kuwa nchi hiyo inaweza kushuhudia "marekebisho makubwa ya muundo wake wa kijamii na kisiasa."

"Kufuatia chaguzi tatu zenye mzozo, serikali ya sasa inaonekana kuwa imeimarisha nguvu zake," alisema. "Kufifia kwa mipaka kati ya serikali, jamii na uchumi, hali iliyoanza na uchaguzi wa upande mmoja wa 2014, kunaweza kusababisha uunganishwaji wake kamili," aliiambia DW.

Soma pia:Sheikh Hasina ashinda tena Bangladesh 

Zakaria alisema matukio kama hayo yanahatarisha kuzidisha mgawanyiko wa kisiasa na msukosuko. "Jambo hili, linalozingatiwa katika mataifa mbalimbali, mara nyingi hugeuka kuwa udikteta wa kisiasa wenye nguvua na kuwa mfumo wa kiimla ambapo kundi maalum linatawala kila nyanja ya dola," alisisitiza.

Inawezaje kuathiri uhusiano wa kidiplomasia wa Dhaka?

Hali hiyo inaweza pia kuwa changamoto kwa baadhi ya uhusiano wa kidiplomasia wa Dhaka, hasa na Marekani. Uhusiano kati ya pande hizo mbili umekuwa wa wasiwasi tangu Washington ilipoapa kuweka vikwazo vya visa kwa yeyote atakayevuruga mchakato wa uchaguzi. Hasina aliishutumu Marekani kwa kujaribu kupanga njama ya kumwondoa madarakani.

Mtaalamu wa Bangladesh Lorch alisema, "kuna muafaka mkubwa nchini Marekani na Ulaya kwamba huu haukuwa uchaguzi wa kidemokrasia."

"EU, kwa mfano, haikutuma ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kwa sababu masharti ya uchaguzi huru na wa haki na ujumbe wenyewe kufanya kazi kwa uhuru haukuwa sawa," alibainisha. "Ukandamizaji wa upinzani kwa ujumla unatambuliwa na kulaaniwa nchini Marekani na katika miji mikuu ya mataifa ya Ulaya."

Maandamano ya vyama vya upinzani Bangladesh
Maandamano ya dhidi ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina.Picha: Mortuza Rashed/DW

Sultan Mohammed Zakaria, mtaalam wa Bangladesh katika shirika la Amnesty International, alidokeza kwamba Marekani tayari imechukua hatua kuiwekea shinikizo Dhaka kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu.

"Marekani imejibu kwa kukiwekea vikwazo Kikosi cha Rapid Action Battalion (RAB) cha Bangladesh na kutekeleza vizuizi vya visa kwa watu wanaotuhumiwa kuhujumu demokrasia," alisema. Lakini, aliongeza, kwamba hatua hizo hadi sasa zimekuwa na athari ndogo.

"Licha ya hatua hizi, uchaguzi ulifanyika na kukosolewa vikali, ikiashiria kuwa mkakati wa sasa wa Magharibi unaweza usiwe na ufanisi,” Zakaria alisema.

Hasina asema uchumi ndio kipaumbele chake

Hasina alisema Jumatatu kuwa maendeleo ya kiuchumi ya Bangladesh ndio kipaumbele chake kikuu katika miaka mitano ijayo. "Kila chama cha siasa kina haki ya kuchukua uamuzi. Kutokuwepo kwa chama kimoja katika uchaguzi haimaanishi kuwa demokrasia haipo," Hasina aliwaambia waandishi wa habari.

Hasina mara nyingi anasifiwa kwa kusimamia ukuaji wa kuvutia wa Bangladesh katika miaka ya hivi karibuni. Lakini uchumi wa nchi hiyo kwa sasa unakabiliwa na matatizo lukuki.

soma pia:Vituo vya kupigia kura vyafunguliwa Bangladesh 

Bei za vyakula na mafuta zimekuwa zikipanda, na kutishia kuwarudisha Wabangladesh wengi kwenye umaskini. Wakati huo huo, akiba ya fedha za kigeni imeshuka hadi chini ya miezi mitatu ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Sekta ya nguo, ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Bangladesh ikichangia karibu asilimia 85 ya dola bilioni 55 katika mauzo ya nje ya kila mwaka, imeshuhudia wimbi la maandamano ya wafanyikazi.

"Hadi sasa, hakuna dalili zozote kwamba serikali ya Awami League itaweza kukabiliana na hali ya kiuchumi. Iwapo ingeweza kupunguza ongezeko la bei ya bidhaa muhimu, kuna uwezekano mkubwa ingefanya hivyo kabla ya uchaguzi ili kupata uungwaji mkono wa wananchi na,"  hivyo, kuboresha uitikiaji katika uchaguzi," Lorch alisema.

"Kama hali ya kiuchumi ya sehemu kubwa ya raia haitaboreka, serikali inaweza kukabiliwa na machafuko ya kijamii, hasa ikiwa upinzani utajiunga na kuzidi kuhamasisha matakwai ya kijamii."