1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya vita Gaza, wakaazi wakabiliwa na masaibu yale yake

24 Mei 2021

Wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Antony Blinken, anaelekea Mashariki ya Kati kuimarisha makubaliano ya kusitisha vita kati ya Hamas na Israel, wakaazi wa Ukanda wa Gaza waanza tena kuyajenga upya maisha yao.

https://p.dw.com/p/3tsY1
Gaza - Israel Konflikt | Waffenstillstand | Bilder der Zerstörung in Gaza
Picha: Ibraheem Abu Mustafa/Reuters

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais Joe Biden, waziri wake huyo wa mambo ya kigeni angelikutana na viongozi wa Israel kuzungumza nao juu ya kujitolea kwa Marekani kwa ajili ya usalama wa taifa hilo la Kiyahudi.

Lakini kwa upande mwengine, Biden anasema amemuagiza Blinken kuendeleza juhudi za kujenga upya mashirikiano na watu na viongozi wa Palestina, ambazo zilikuwa zimeachwa kipindi kirefu na utawala wa mtangulizi wake, Donald Trump.

Ziara hii ya Blinken inafanyika katika wakati ambapo kiwango cha ukosoaji wa ndani na nje dhidi ya siasa ya Marekani kuelekea Mashariki ya Kati kikiwa cha juu, hasa kufuatia mashambulizi ya karibuni ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Soma pia: Waisraeli na Wapalestina waanza kurudia maisha ya kawaida

Ndani ya chama chake cha Democratic, viongozi kadhaa wamemshutumu waziwazi Biden kwa kuendelea na mpango wa kuiuzia silaha Israel katika wakati ambapo watoto 66 wasio na hatia waliuawa.

Gaza - Israel Konflikt | Waffenstillstand | Bilder der Zerstörung in Gaza
Mwanamke wa Kipalestina akiondoa vitu vyaka vilivyosalimika baada ya kurejea nyumbani kwenye nyumba yake iliyoharibiwa na kusalia vifusi.Picha: Ibraheem Abu Mustafa/Reuters

Hao ni miongoni mwa Wapalestina 248 waliouawa na wengine 1,900 waliojeruhiwa, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza. Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya nusu ya waliouwa kwa makombora ya Israel walikuwa raia wa kawaida.

Makombora ya Hamas kuelekea Israel yaliuwa watu 12, akiwemo mtoto mmoja na mvulana mwenye asili ya Kiarabu, mwanajeshi mmoja, raia mmoja wa India na wawili wa Thailand. Watu 357 walijeruhiwa kwa upande wa Israel.

Dhana ya madola mawili kama suluhisho pekee

Biden alisema kwamba nchi yake inataka kujihusisha kwenye diplomasia ya kiwango cha juu kukomesha uhasama na kupunguza hali ya wasiwasi baina ya Israel na Wapalestina, huku Blinken akisema Marekani inaunga mkono uundwaji wa madola huru kama njia pekee ya kuwarejeshea matumaini Waisraeli na Wapalestina kwamba wanaweza kuishi pamoja kwa amani, usalama, na heshima.

Soma pia: Umoja wa Mataifa: Watu 800,000 Gaza hawana maji safi

Lakini je, ni kwa kiasi gani mtazamo wa Marekani kuelekea eneo la Mashariki ya Kati unayagusa maisha kama ya Ramez al-Masri, mkaazi wa Gaza, ambaye ilimchukuwa miaka mitatu kuijenga upya nyumba yake baada ya kubomolewa na mashambulizi yaIsrael mwaka 2014, na yaliporejea tena wiki iliyopita, ilichukuwa sekunde chache tu kuigeuza tena kifusi?

Hali ya Ramez ndiyo waliyonayo maelfu ya Wapalestina wenzake walioachwa bila makaazi kutokana na mashambulizi mengine ya Israel. Yeye na wenzake wengine 16 waliokuwa wakiishi kwenye nyumba ya ghorofa mbili wataendelea kukosa mahala pa kukaa hadi hapo msaada wa kimataifa utakapokuja kuwasaidia kujenga tena nyumba.

Gaza - Israel Konflikt | Waffenstillstand | Bilder der Zerstörung in Gaza
Wapalestina wakipumzika kwenye vifusi baada ya kurejea kwenye nyumba yao iliyoharibiwa kufuatia mapatano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.Picha: Mohammed Salem/Reuters

"Wanangu wametawanyika - wawili kule, watatu hapa, mmoja pale. Mambo kwa kweli ni magumu sana. Tunaishi kwenye mdomo wa mauti kila siku, madhali tupo kwenye ukaliwaji wa kimabavu," anasema akimaanisha utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina, ukiwemo mzingiro wa Gaza.

Soma pia: Kwa nini Umoja wa Ulaya hauna ushawishi Mashariki ya Kati?

Umoja wa Mataifa unakisia kwamba kiasi cha nyumba 1,000 zimebomolewa kabisa kabisa kwenye Ukanda wa Gaza. Mratibu wa Umoja huo, Lynn Hastings, anasema mamia ya nyumba nyengine zimebomolewa kwa kiwango ambacho haziwezi tena kukaliwa.

Hamas, Israel waanza makubaliano usitishaji mapigano

Hata hivyo, madhara ya mashambulizi ya siku 11 mara hii hayakuwa makubwa kama yale ya siku 50 mwaka 2014, ambapo viunga vizima vilibomolewa na jumla ya nyumba 141,000 ama zikageuzwa vifusi au kuharibiwa vibaya mno.

Lakini, baada ya mashambulizi hayo ya 2014, wafadhili wa kimataifa walijitokeza haraka na msaada wa dola bilioni 2.7 kuijenga upya Gaza. Safari hii, kutokana na dunia kukabiliwa na janga la COVID-19 na miaka kadhaa ya kushindwa kwa diplomasia, hakuna uhakika ikiwa wafadhili watakubali tena kuingiza mikono mifukoni mwao na kumimina fedha za kuijenga Gaza.

Vyanzo: AP/AFP