1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Azimio la kupinga mzingiro wa mji wa Al-Fashir kupigiwa kura

13 Juni 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa leo kulipigia kura azimio lililotayarishwa na Uingereza linalotaka kufikia mwisho kwa mzingiro wa mji wa Al-Fashir uliopo kwenye mkoa wa Darfur Kaskazini nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4gyW5
Mapigano kwenye mji wa Al-Fashir nchini Sudan
Mapigano kwenye mji wa Al-Fashir nchini Sudan. Picha: AFP

Mji huo umezingirwa na vikosi vya wanamgambo wa RSF vinavyopigana na jeshi la Sudan kuwania madaraka ya nchi hiyo.

Rasimu ya azimio hilo ambayo shirika la habari la Reuters imeiona, inatoa mwito pia wa kusitisha mara moja mapigano, kukomesha makabiliano ndani na kwenye viunga vya mji huo pamoja na kuondoka kwa wapiganaji wote wanaotishia usalama wa raia. Uingereza imependekeza kura hiyo ipigwe leo mchana.

Azimio lenyewe litahitaji angalau kura 9 za kuliunga mkono na bila kuwepo kura ya turufu ya kulipinga kutoka miongoni mwa nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama.