Athari kiuchumi kwa Afrika kufuatia mzozo wa Ukraine
16 Machi 2022Kuanzia mashirika ya ndege nchini Nigeria hadi wanunuzi wa bidhaa nchini Malawi, Waafrika wanakabiliwa na athari za mzozo wa Ukraine hususan, ongezeko la bei ya bidhaa, mathalan mafuta, nafaka na mbolea.
Bei ya mafuta ulimwenguni imepanda kwa zaidi ya dola 100 tangu Februari 24 wakati Urusi ilipoivamia Ukraine. Hilo likiwa ongezeko la juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo mingi. Hali hiyo imeathiri pakubwa shughuli nyingi za kibiashara kusini mwa jangwa la Sahara.
Soma pia: Viongozi watatu wa Ulaya wafanya ziara Ukraine
Ukraine na Urusi ni nchi zinazoongoza katika uzalishaji wa ngano na nafaka nyinginezo zinazouzwa Afrika. Aidha Urusi ni taifa linalotengeneza mbolea kwa kiwango kikubwa.
Athari ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, pamoja na vikwazo vya nchi za magharibi kwa Urusi, tayari vimeanza kusababisha kupanda kwa bei ya pembejeo na nafaka zinazoagizwa Afrika kutoka mataifa ya nje. Hayo ni kulingana na ripoti ya matawi mbalimbali ya shirika la habari la AFP barani Afrika.
Athari nchini Kenya
Nchini Kenya, paketi ya kilo mbili ya ngano iliyokuwa ikiuzwa kati ya shilingi 150-170) ambayo ni sawa na dola moja na senti tatu mnamo mwezi Februari, sasa imepanda bei kwa shilingi 140 zaidi.
Soma pia: Baa la njaa linanukia kutokana na kupanda bei za vyakula tangu Urusi ilipoivamia Ukraine
Nchi hiyo ambayo uchumi wake ni namba tatu miongoni mwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, huagiza moja juu ya tano ya ngano inayotumia kutoka Urusi huku ikiagiza asilimia 10 ya bidhaa hiyo kutoka Ukraine. Hayo ni kulingana na data za serikali.
Mfuko mmoja wa kilo 50 za mbolea, ambayo kawaida huuzwa shilingi 4,000, sasa inauzwa shilingi 6,500.
Kampala Uganda
Nchini Uganda, katika mji mkuu Kampala, mzozo wa Ukraine pia umesababisha bei ya sabuni, chumvi, mafuta ya kupikia na nishati kupanda.
David Bahati ambaye ni waziri msaidizi katika wizara ya fedha ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, nyingi ya bidhaa muhimu huzalishwa nchini humo. Lakini viungo vingine huagizwa kimataifa na bei ya viungo hivyo kwa sasa zimepanda.
Kwa mfano mafuta ya kupikia imepanda kutoka shilingi za Uganda 7,000 hadi 8,500 huku bei ya mpunga ikipanda kutoka 3,800 hadi 5,500. Hayo ni kulingana na muuzaji mmoja kwenye duka mjini Kampala.
Rita Kabalu mkaazi wa Kampala mwenye umri wa miaka 41 ameliambia AFP kwamba kwa wastan familia yake hutumia shilingi 5,000 kununua mahitaji yao ya kila wiki. Lakini kwa sasa wanatumia 1,000 zaidi.
Sekta ya nishati Nigeria yaathiriwa
Julius Adewale ambaye ni muokaji wa mikate mjini Lagos Nigeria, anasema mzozo huo umevuruga pakubwa biashara.
Katika siku za hivi karibuni, mitambo ya nishati nchini Nigeria hutoa kiasi kidogo tu cha umeme kila siku. Hali hiyo imemlazimisha Adewale kutumia jenereta yake inayotumia mafuta aina ya dizeli lakini hata bei ya dizeli nayo imepanda.
"Hatujakuwa na umeme tokea jana, hivyo tumekuwa tukitumia jenereta. Gharama ya uokaji imeongezeka mno,” amesema Adewale huku wafanyakazi wakipakua mikate kwenye kreti.
Nigeria ndiyo nchi inayoongoza katika uchimbaji mafuta barani Afrika na vile vile ndiyo nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani humo. Lakini uwezo wake wa kusafisha mafuta hayo ni mdogo.
Mashirika ya ndege yapunguza idadi ya ndege safarini
Serikali hupunguza bei ya petroli lakini dizeli na mafuta ya ndege huuzwa kalingana na bei ya kimataifa.
Mashirika kadhaa ya ndege barani Afrika yametahadharisha mwezi huu kuwa yatalazimika kufuta baadhi ya safari za ndege kufuatia uhaba wa mafuta.
Nchini Nigeria, dizeli ilikuwa ikiuzwa Naira 300, ambayo ni sawa na dola senti 72 kwa kila lita. Lakini kwa sasa lita moja inauzwa naira 730 sawa na dola moja na senti 75.
Lanrte Popoola, mwenyekiti wa chama cha viwanda Nigeria ameviambia vyombo vya habari nchini humo kwamba hawajui namna wataendeleza shughuli zao.
"Biashara nyinginezo zimepunguza muda wa operesheni za mashine zao kwa sababu haziwezi kumudu bei ya juu ya dizeli,” amesema Popoola.
"Ikiwa mzozo huu utaendelea basi nchi za Afrika ambazo kwa kawaida huagiza pakubwa bidhaa nyingi za mafuta na ngano, zitapata hasara kubwa, na wauzaji wa bidhaa hizo huenda wakapata faida zaidi,” amesema Amaka Anku, mchambuzi wa masuala ya kiuchumi kutoka shirika la Eurasia.
Nchi zinazoweza kufaidika ni zipi?
Nchi zinazovuna gesi mfano Tanzania, Senegal na Nigeria huenda zikanufaika kutokana na hatua ya nchi za Ulaya kupiga marufuku mafuta na gesi kutoka Urusi. Hayo ni kwa kulingana na Danielle Resnick kutoka shirika la utafiti la Brookings.
Lakini ameongeza kuwa changamoto ya moja kwa moja kwa sasa ni ugumu unaozikumba familia za Afrika kwa sasa kufuatia athari za mzozo huo.
Mnamo Jumapili, mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani IMF, Kristalina Georgieva alisema vita nchini Ukraine vinamaanisha njaa kwa Afrika.
Bei ya juu ya bidhaa hukosesha zaidi usalama wa chakula hasa katika maeneo yaliyokuwa yakikumbwa na machafuko kama Ethiopia ambapo takriban watu milioni 20 wanahitaji chakula cha misaada.
Ghana, Mauritius, Somalia hadi Malawi ni miongoni mwa nchi barani Afrika ambazo vilio vya watu kufuatia kupanda kwa bei ya bidhaa vimesikika. Na yote ni kutokana na mzozo wa Ukraine ambao licha kuwa ni mbali na Afrika, athari zake zinashuhudiwa kwingi ulimwenguni.