1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askofu Mkuu Robert Zollitsch aomba radhi tena.

Abdu Said Mtullya12 Machi 2010

Kiongozi wa kanisa katoliki nchini Ujerumani Robert Zollitsch leo amekutana na Baba Mtakatifu Benedikt wa 16.

https://p.dw.com/p/MRUr
Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 akimsikiliza kiongozi wa kanisa katoliki nchini Ujerumani, Robert Zollitsch.Picha: picture alliance/dpa

Kiongozi wa kanisa katoliki nchini Ujerumani Askofu Mkuu Robert Zollitsch kwa mara nyingine ameomba radhi juu ya mikasa ya kuharibiwa kwa watoto wa kiume na makasisi kwenye taasisi mbalimbali za kanisa katoliki.

Askofu Mkuu Zollitsch amechukua hatua hiyo leo baada ya kukutana na Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 kwenye makao makuu ya kanisa Katoliki ya Vatikan.Kiongozi huyo wa wakatoliki wa Ujerumani amesema Baba Mtakatifu amempa moyo juu ya kuchukua hatua ili kukabiliana na tatizo hilo.Amesema kanisa katoliki nchini Ujerumani linachukua hatua katika kutoa ushauri kwa watu waliodhalilishwa na makasisi pamoja na kuyafanyia uchunguzi madai juu ya kudhalilishwa kwa watu hao. Askofu Mkuu Zollitsch ameeleza kwamba lengo la hatua hizo ni kuepusha kutokea tena kwa mikasa kama hiyo.

Hata hivyo ametamka kuwa uharibifu wa watoto hautokei katika kanisa katoliki tu.!Lakini ameahidi kuwa kanisa hilo nchini Ujerumani litashirikiana na idara za sheria.

Askofu mkuu huyo amesema kuwaharibu watoto wa kiume kingono ni uhalifu wa kuchukiza sana.Mnamo siku za hivi karibuni palifichuka habari juu ya uhalifu wa kuharibiwa watoto wa kiume kwenye makanisa ya Ujerumani.Wanafunzi wasiopungua 170 kutoka kwenye shule za kanisa katoliki nchini Ujerumani walijitokeza hivi karibuni na kutoa madai juu ya kudhalilishwa kingono na kufanyiwa vitendo vya nguvu. Madai hayo yametolewa pia na wanafunzi wa kwaya maarufu ya Regensburg ya watoto wa kiume iliyowahi kuongozwa na nduguye Baba Mtakatifu Benedekt XVI.

Kiongozi wa kanisa katoliki la Ujerumani askofu Mkuu Zollitisch alikutana na Baba Mtakatifu kwa dakika 45 kwenye makao ya Vatikan leo.Aliwaambia waandishi habari baada ya mkutano huo kwamba Baba Mtakatifu alipokea kwa mshtuko na huzuni kubwa habari juu ya madai ya uhalifu waliotendewa watoto wa kiume kwenye taasisi za kanisa katoliki nchini Ujerumani.

Askofu Zollitsch amesema Baba Mtakatifu anaunga mkono kwa moyo wote hatua zinazochukuliwa sasa nchini Ujerumani ili kushughulikia mikasa iliyotokea mnamo miaka ya nyuma na kuzuia kutokea kwa mikasa mingine kama hiyo mnamo siku za usoni.

Askofu Zollistch amesema anataka ukweli ujulikane kwa sababu waliotendewa uhalifu wana haki ya kujua ukweli huo. Kanisa katoliki la Ujerumani limemteua Askofu atakaesimamia mikasa inayohusu kuharibiwa kwa watoto makanisani.

Mwandishi/Mtullya Abdu/ /afp/ dpa/ZA

Mhariri/ Josephat Charo