1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asilimia 50 ya wazee Tanzania bado ni walezi wa watoto

28 Septemba 2018

Tafiti zinakadiria kuwa zaidi ya 50% ya wazee nchini Tanzania wanakabiliwa na malezi ya watoto na hali ngumu ya kimaisha, hali inayowalazimisha kuendelea kufanya shughuli za kiuchumi badala ya kupumzika.

https://p.dw.com/p/35eMz
Alzheimer und Pflege
Picha: Colourbox

Sera ya taifa ya wazee ya mwaka 2003 nchini Tanzania inamtafsiri mzee kuwa ni mtu mzima anayeanzia miaka 60 na kuendelea.

Huu ni umri ambao mtu huyu anastahili kupumzika kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuangaliwa kwa ukaribu na jamii yake ikiwemo serikali.

Lakini mambo yamebadilika katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ambalo kundi hili linatajwa kuachiwa jukumu kubwa la malezi ya watoto ilhali wenyewe walikuwa ndio wanastahili kulelewa.

Kwa mfano, Bi Khadija anayeishi mtaa wa Azimio wilaya ya Handeni mkoani Tanga anasema ana wajukuu ishirini na saba, wanne wakiwa wamefariki, huku anaowalea mwenyewe wakiwa zaidi ya watano.

Bi Khadija anasema hali ya maisha kwake inazidi kuwa ngumu siku hadi siku kutokana na mzigo wa familia unaomkabili.

Tanzania inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 45 na, kwa mujibu wa sera ya taifa ya wazee, kuna wazee milioni 1.4, ambao ni sawa na 4% ya wakaazi wote.

Lakini, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, kuwa zaidi ya 50% ya wazee hawa wanakabiliwa na malezi ya watoto, ikiwemo mayatima.

Bi Mariam ni mmoja wao. Yeye alizaliwa mwaka 1953, anaishi katika kijiji cha Msasa. "Mume wangu alifariki miaka mitano iliyopita. Hapa nalea wajukuu zake watatu ambao mama yao anafanya kazi katika mashamba ya mkonge mbali na hap," anasema Bi Mariam akiongeza kuwa licha ya kutumiwa fedha na mwanawe kuwalea watoto hao, mara kadhaa hali hukwama ama na yeye huokoa jahazi.

Serikali, hata hivyo, inasema ina mfumo madhubuti wa kijamii ambao, kwa mujibu wa Afisa Ustawi wa Jamii katika wilaya ya Handeni, Bwana Frank, unaziokoa kaya masikini kiuchumi.

"Serikali hizi za wilaya ndizo zilizopewa majukumu ya kisheria na kisera kuwaangalia wazee na kuhakikisha kuwa wanakuwa salama," anasema mkuu wa wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe.

Mwandishi: Hawa Bihoga/DW Tanga
Mhariri: Josephat Charo