Arsene Wenger kuachia ngazi mwishoni mwa msimu
20 Aprili 2018Wenger mwenye umri wa miaka 68 alishinda mataji matatu ya Premier League na vikombe saba vya kombe la FA katika kipindi cha miaka 22 akiwa katika uongozi wa timu ya Arsenal lakini misimu ya hivi karibuni imeamsha hali ya kutoridhika miongoni mwa mashabiki wakati klabu hiyo ilishindwa kupambana kuwania taji la ligi.
Tony Adams , nahodha wa Arsenal wakati timu hiyo iliposhinda ligi kuu ya England Premier League na kombe la FA msimu wa mwaka 1997 / 98 na tena mwaka 2003 / 04 hana shaka kuhusiana na nafasi ya kihistoria ya kocha wake huyo wa zamani katika klabu hiyo ya mjini London. "Ahsante kwa kila kitu Arsene. Adams aliandika katika ukurasa wa Instagram.
Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amesema "ameshangaa" alipokuwa akizungumza na waandishi habari.
"Alikuwa mtu aliyetamalaki katikati ya miaka 1990 na 2000" Klopp alisema katika mkutano wake na waandishi habari siku ya Ijumaa. "Ni tofauti hivi sasa kwasababu tunapaswa kutoa changamoto lakini nchini Ujerumani alikuwa mtu wa mfano mkubwa," aliongeza kocha huyo raia wa Ujerumani.
Raia huyo wa Ufaransa anaondoka katika uongozi wa Arsenal mwaka mmoja kabla ya kumalizika kwa mkataba wake wa hivi sasa wa miaka miwili. Arsenal iko nafasi ya sita katika Premier League na imo katika nusu fainali ya kombe la ligi ya Ulaya, Europa League.
Kila la kheri Wenger
"Baada ya kutafakari kwa kina na kufuatia majadiliano na klabu , nahisi ni muda sahihi wa kuondoka mwishoni mwa msimu," Wenger alisema katika taarifa.
Mmiliki wa hisa kubwa katika Arsenal Stan Kroenke alisema klabu itamteua kocha mpya haraka iwezekanavyo.
"Hii ni moja kati ya siku ngumu sana katika miaka yote katika spoti, " alisema katika taarifa ya klabu chini ya kichwa cha maneno "Mercy Arsene" akiwa na maana ahsante Arsene.
Wenger aliteuliwa Oktoba 1, 1996 na kwa sasa ni kocha aliyetumikia kwa muda mrefu zaidi katika Premier League.
"Chochote kitakachokuja hapo baadaye kwake, hastahili pungufu ya shukrani zetu za dhati na kumtakia kila la kheri kwa maisha yake ya furaha."
Katika mwaka 2003-04 , Wenger alikuwa kocha wa kwanza tangu mwaka 1888-89 kuiongoza timu katika msimu mzima wa ligi ya juu bila kufungwa.
"Katika mwaka huo tulikuwa tunajaribu tu kuwa mabingwa," Thierry Henry , mfungaji mashuhuri wa klabu hiyo aliiambia televisheni ya michezo ya Sky.
"Alikuwa anatuambia wakati tayari ni mabingwa, "vijana mnaweza kufanya kitu cha kushangaza."
Wenger alishinda taji lake la saba la kombe la FA msimu uliopita, wakati Arsenal ikiishinda Chelsea kwa mabao 2-1 uwanjani Wembley, lakini kikosi chake kilishindwa kufikia kucheza katika Champions League kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 17, na kumekuwa na hali ya kutoridhika miongoni mwa sehemu ya mashabiki wa Arsenal, ambao wamekuwa wakitoa miito ya Wenger kuondoka.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae