1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annalena Baerbock azuru India

5 Desemba 2022

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock ameanza leo ziara ya siku mbili nchini India inayolenga kupigia upatu umuhimu wa kuheshimiwa maadili ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/4KTwx
Indien Neu Delhi | Außenministerin Baerbock und Außenminister Subrahmanyam Jaishankar
Picha: Carsten Koall/dpa/picture alliance

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock ameanza leo ziara ya siku mbili nchini India inayolenga kupigia upatu umuhimu wa kuheshimiwa maadili ya kimataifa pamoja na masuala mengine yenye maslahi kwa pande mbili.

Muda mfupi baada ya kuwasili mjini New Delhi, bibi  Baerbock na ujumbe wake walilitembelea eneo la kumbukumbu ya Mahatma Gandhi, aliyekuwa mwanaharakati mashuhuri wakati wa harakati za kupigania uhuru wa India kutoka kwa Uingereza.

Baadaye leo mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani amepangiwa kuwa na mazungumzo na mwenzake wa India , Subrahmanyam Jaishankar.

Kabla ya kusafiri kuelekea New Delhi, Baerbock alisema katika wakati ulimwengu unakabiliwa na vita pamoja na kitisho cha kutanuka kwa nguvu za China, ziara yake nchini India italiweka mezani kwa umuhimu mkubwa suala la ulazima wa mataifa yote kuheshimu kanuni za kimataifa.