1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANKARA : Mazungumzo ya Uturuki na Umoja wa Ulaya mashakani

30 Septemba 2005
https://p.dw.com/p/CEWN

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Abdullah Gul amesema mazungumzo ya nchi yake kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya huenda yasianze hapo Jumaatatu kama ilivyopangwa.

Gul amewaambia waandishi wa habari mjini Ankara kwamba Uturuki haitopeleka ujumbe wake huko Luxembourg kabla ya kwanza kuona waraka wa Umoja wa Ulaya wenye kuainisha mfumo wa mazungumzo hayo.Uturuki mara kwa mara imekuwa ikisema kwamba haitokubali chochote kile pungufu ya kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya ikiwa kama ni lengo lililotamkwa la mazungumzo hayo.

Hata hivyo Austria nchi mwanchama wa Umoja wa Ulaya imesema iko tayari tu kukubaliana na mazungumzo hayo kwa Uturuki kupatiwa ushirika wa upendeleo maalum na Umoja wa Ulaya.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama 25 wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kuwa na mkutano wa dharura huko Luxembourg hapo Jumapili kwa lengo la kuondosha kikwazo hicho.