1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angela Merkel kuachia ngazi 2021

Daniel Gakuba
29 Oktoba 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza kuwa hatagombea tena uongozi wa chama chake cha Christian Democratic Union -CDU, na kwamba muhula wa sasa wa ukansela ambao ni wa nne madarakani utakuwa wake wa mwisho.

https://p.dw.com/p/37LUG
Berlin Merkel-Pressekonferenz nach Hessen-Wahl
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Kansela Merkel ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari katika makao makuu ya chama chake mjini Berlin, akiongeza kuwa muda umewadia wa kufungua ukurasa mpya. Merkel mwenye umri wa miaka 64 amekuwa mwenyekiti wa chama cha CDU tangu mwaka 2000, na Kansela wa Ujerumani tangu mwaka 2005. Katika kipindi cha miaka 13 kama Kansela, amekuwa pia kileleni mwa siasa za Ulaya.

Bi Merkel amegusia mivutano ya ndani ya vyama vinavyounda mseto wa serikali anayoiongoza, ambayo imesababisha mzozo baada ya mwingine, na kuhitimisha kwamba taswira inayotoka katika serikali hiyo haikubaliki. Kwa hatua ya kujiweka kando, Merkel amesema anatoa mchango wa kuwepo ufanisi zaidi serikalini.

Angela Merkel und Annegret Kramp-Karrenbauer
Annegret Kramp-Karrenbauer (kushoto) ambaye anapewa nafasi ya kumrithi Kansela Merkel.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

''Kwa uamuzi huu najaribu kuchangia katika kuiwezesha serikali ya Ujerumani, hatimaye kujikita katika juhui za uongozi bora, suala ambalo wananchi wamekuwa wakikidai, kitu ambacho ni haki yao,'' amesema Merkel na kuendelea,  ''Hatua hii vile vile inakwenda sambamba na azma ya serikali ya Ujerumani kufanya tathmini ya nusu muhula, kuhusu ilivyotekeleza majukumu yake, kama ilivyokubaliwa na vyama vya CDU, CSU na SPD katika mkataba wa kuunda serikali ya mseto.''

Mwanzo wa mwisho wa Merkel katika siasa za Ujerumani na dunia

Hii ina maana kwamba jina la Angela Merkel halitakuwa katika orodha ya wanaogombea uenyekiti wa CDU katika mkutano mkuu wa chama hicho mjini Hamburg Desemba mwaka huu, wala kwenye uchaguzi wa ukansela mwaka 2021. Aidha, Bi Merkel amesema katika tangazo lake, kwamba baada ya kuachia wadhifa wa ukansela, hatagombea nafasi yoyote nyingine ya kisiasa.

Infografik Landtagswahlen Hessen 2018 Sitzverteilung EN
Vyama vikuu vya Ujerumani vimekuwa vikipoteza kura katika uchaguzi wa shirikisho na wa kimajimbo

Mwanasiasa huyo wa Ujerumani ambaye alikuwa akichukuliwa kama mwanamke mwenye nguvu zaidi duniani, na mwenye kauli ya mwisho katika Umoja wa Ulaya, alianza kupoteza ushawishi baada ya uamuzi wake wa kuruhusu wakimbizi zaidi ya milioni moja kuingia nchini Ujerumani mwaka 2015.

Ukarimu wake kwa wakimbizi wamponza

Mminiko huo wa wakimbizi ulileta mgogoro katika siasa za Ujerumani, na unaaminika kuwa sababu ya kuimarika kwa siasa za mrengo mkali wa kulia, hususan chama cha Mbadala kwa Ujerumani -AfD.

Gazeti la Die Welt la hapa Ujerumani limebashiri kuwa kujiondoa kwa Merkel kunamsafishia njia Katibu Mkuu wa CDU Annegret Kramp-Karrenbauer, maarufu kama AKK kurithi mikoba yake. Lakini wapo wengine wanaoinyemelea nafasi hiyo, akiwemo mkosoaji mkubwa wa Bi Merkel Jens Spahn ambaye pia ni waziri wa afya.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman