1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

ANC yaelekea kupoteza wingi wa kura Afrika Kusini

30 Mei 2024

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Afrika Kusini huku matokeo ya awali kutoka baadhi ya maeneo ya taifa hilo yakionyesha chama African National Congress, ANC kupoteza wingi wa viti bungeni.

https://p.dw.com/p/4gRxo
Afrika Kusini | Uchaguzi
Zoezi la kuhesabu kura likiendelea katika shule ya msingi ya Craighall Park huko Johannesburg, Afrika Kusini.Picha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Matokeo ambayo yanaweza kuwa mabadiliko makubwa ya kisiasa tangu mwisho wa ubaguzi wa rangi.

Kulingana na takwimu za tume ya uchaguzi, kufikia sasa asilimia 11.3 ya kura zimeshahesabiwa, na chama cha ANC kimepata asilimia 42.8 ikifuatiwa na chama cha kileberali cha Democratic Alliance kwa asilimia 26.5 ya kura huku chama cha mwanasiasa Julius Malema cha Economic Freedom Fighters EFF kikichukua nafasi ya tatu kwa asilimia 8.3.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuhesabu kura Nombuyiselo Biyela, msimamizi wa kituo kimoja cha kupigia kura katika mji wa Eshowe, jimbo la KwaZulu Natal, amesema;

Kwa kweli hatuwezi kusema itachukua muda gani lakini kwa makadirio yetu, haipaswi kuchukua muda mrefu sana kwa sababu tulihifadhi rekodi za takwimu zetu siku nzima. Sasa ni jukumu letu kuona jinsi mchakato unavyokwenda kwa sababu hatujui kama tuna kura zilizoharibika au la. Kwa hivyo, itabidi tusubiri na tuone itachukua muda gani."

Soma pia: ANC yamsimamisha uanachama Zuma baada ya kuunga mkono chama kipya

Ikiwa matokeo ya mwisho yatafuata takwimu za awali,  ANC italazimika kufanya makubaliano na chama kimoja au zaidi kuunda serikali ya mseto, hali ambayo inaweza kuongeza joto la kisiasa katika wiki au miezi kadhaa ijayo nchini Afrika Kusini.

Mazingira magumu kwa ANC

Uchaguzi Africa Kusini 2024 | Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akipiga kura wakati wa uchaguzi wa Afrika Kusini huko Soweto.Picha: Oupa Nkosi/REUTERS

Huku ANC bado ikisalia kuwa chama kikubwa zaidi, kiongozi wake Cyril Ramaphosa huenda akasalia kuwa rais wa nchi hiyo, ingawa matokeo duni yanaweza kumfanya awe katika mazingira magumu na kukabiliwa na changamoto ya uongozi ndani ya chama chake.

Kwa mujibu wa sheria, tume ya uchaguzi ina siku saba kutangaza matokeo kamili, lakini kwa kawaida zoezi hilo hukamilika kabla ya muda ulioratibiwa. Kwa mfano katika uchaguzi uliopita, mnamo 2019, upigaji kura ulifanyika Jumatano

na matokeo ya mwisho yalikuja Jumamosi.

Bunge jipya lazima likutane ndani ya siku 14 baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa na jukumu lake la kwanza ni  kumchagua rais.

ANC imekuwa ikishinda uchaguzi wa kitaifa unaofanyika kila baada ya miaka mitano tangu uchaguzi mkuu wa 1994, ulioashiria mwisho wa ubaguzi wa rangi ambapo Nelson Mandela alichaguliwa  kuwa rais.

Lakini tangu wakati huo uungwaji mkono wa ANC umepungua kutokana na raia kukatishwa tamaa na masuala kama vile ukosefu mkubwa wa ajira, uhalifu, kukatika kwa umeme mara kwa mara na rushwa.

Katika jimbo la KwaZulu-Natal, mkoa wa mashariki wenye watu wengi, chama kipya kinachoongozwa na rais wa zamani Jacob Zuma, Mkhonto we Sizwe (MK), kimejizolea asilimia 42.3 ya kura dhidi ya 20.1 kwa  ANC.

Zuma alilazimika kujiuzulu kama rais mwaka wa 2018 baada ya mfululizo wa kashfa na tangu wakati huo ametofautiana na uongozi wa ANC.