1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AMSTERDAM Uholanzi yaipigia kura ya maoni katiba ya Umoja wa Ulaya

1 Juni 2005
https://p.dw.com/p/CF7z

Waholanzi leo hii wameanza kupiga kura ya maoni juu ya katiba ya Umoja wa Ulaya, huku maoni ya wapigaji kura yakidhidirisha kupingwa kwa katiba hiyo. Iwapo Uholanzi nayo itaikataa katiba hiyo, itazidi kuutumbukiza umoja wa Ulaya katika mzozo wa kisiasa kufuatia hatua ya wafaransa kuipinga katiba hiyo Jumapili iliyopita.

Waziri mkuu wa Uholanzi Jan Peter Balkenende amewatolea wito wapigaji kura wasiopungua milioni 12 kuiunga mkono katiba hiyo. Uchunguzi uliofanywa nchini humo unaonyesha kwamba asilimia 59 kati yao wataipinga. Serikali ya Uholanzi hailazimiki kuyafuata matokeo ya kura hiyo, kama ilivyokuwa nchini Ufaransa, lakini huenda ikalitikisa bunge ambalo lina mamlaka ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Tayari mataifa tisa wanachama wa jumuiya ya Ulaya yameiidhinisha katiba hiyo, lakini ni lazima ipitishwe na mataifa yote 25 wanachhama.

Hatua ya Ufaransa kuikataa katiba hiyo kulilazimisha mabadiliko katika baraza la mawaziri hapo jana, huku Dominiqu de Villepin akiichukua nafasi ya Jean-Pierre Raffarin kama waziri mkuu mpya.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya walioitayarisha katiba hiyo kwa muda wa miaka mitatu watafanya mkutano wa kilele katikati ya mwezi Juni.