1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Zaidi ya waandamanaji 100 wameuwawa Iran

20 Novemba 2019

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limesema zaidi ya watu 100 wameuwawa kwenye miji 21 nchini Iran wakati wa machafuko yaliyozuka wiki iliyopita kupinga kupanda kwa bei ya mafuta.

https://p.dw.com/p/3TMUC
Iran Protest Benzinpreise
Waandamanaji nchini IranPicha: FARS

Katika taarifa iliyochapishwa jana, shirika hilo limesema polisi wa kulenga shabaha walifyetua risasi kuelekea makundi ya waandamanaji kutoka juu ya majengo na katika kisa kimoja kutoka ndani ya helikopta.

Shirika hilo lenye makao yake mjini London limesema taarifa yake ni kutoka duru za kuaminika na vyanzo vingine ikiwemo mashuhuda, kanda za video na maelezo ya watetezi wa haki za raia.

Amnesty imesema vikosi vya polisi na intelejensia havikurudisha miili ya waliuwawa kwa familia zao na vimelazimisha baadhi ya miili kuzikwa haraka bila kufanyiwa uchunguzi wa kitababu.

Taarifa hiyo imefichua jinsi vikosi vya usalama nchini Iran vinavyoendesha mauaji ya raia kinyume na sheria ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu katili na nguvu iliyopindukia.

Raha Behreini, ambaye ni mwanasheria na mtafiti wa Amnesty International amesema "Mamlaka za Iran zina historia ya kutumia ukatili na nguvu kubwa dhidi ya wale wanatimiza haki yao ya kujieleza na kuandamana kwa amani. Hata hivyo inaonekana mara hii, wamezidisha zaidi ukandamizajai kwa sababu hawataki maandamano hayo yawe makubwa"

Huduma ya Intaneti yaendelea kuzimwa

Iran Proteste gegen Erhöhung der Benzinkosten
Raia wa Iran akionesha maganda ya risasi zilizofyetuliwa na polisiPicha: picture-alliance/abaca/SalamPix

Iran yenyewe haijatoa taarifa ya idadi ya watu waliokamatwa, kujeruhiwa au kuuliwa wakati wamaandamano hayo yaliyosambaa haraka kwenye karibu majiji na miji 100.

Mamlaka nchini humo zimezima huduma za mtandao wa intaneti tangu siku ya Jumamosi na hali hiyo imeendelea hadi jana jumanne.

Kukosekana kwa upatikanaji taarifa kumevifanya vyombo vya habari vya Iran na maafisa wa nchi hiyo pekee kuwa na uwezo wa kutoa taarifa kuhusu kinachoendelea.

Afisa mmoja nchini Iran amesema maandamano hayo yamepungua nguvu baada ya kikosi cha ulinzi wa mapinduzi cha jeshi la Iran kutishia kuchukua hatua kali iwapo yataendelea.

Kwanini kumekuwa na ongezeko la bei ya mafuta?

Iran Ruhani verurteilt «Gewalt und Vandalismus» bei Protesten
Kituo hiki cha mafuta kilichomwa moto wakati wa maandamanoPicha: AFP

Maandamano dhidi ya serikali nchini Iran yalianza Ijumaa iliyopita baada ya tangazo la kupandishwa kwa bei za mafuta kwa asilimia 50.

Kupanda kwa bei ya mafuta kunamaanisha kuwa chanagmtoo nyingine kwa raia wa nchi hiyo ambao tayari wameathiriwa na kuanguka kwa sarafu ya nchi hiyo.

Hali imezidi kuwa mbaya nchini humo tangu utawala wa rais Donald Trump kuitoa Marekani kutoka mkataba wa nyuklia wa Iran na madola yenye nguvu na kurejesha vikwazo vinavyoulemeza uchumi wa Iran.

Rais wa Iran aliye na msimamo wa wastani Hassan Rouhani aliahidi kuwa nyongeza ya bei ya mafuta itatumika kutoa ruzuku na marupurupu zaidi kwa familia masikini.

Hata hivyo uamuzi huo umezusha hasira kubwa miongoni mwa raia wa taifa hilo la Kiislam.