1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Serikali haziwalindi wahudumu wa afya na corona

13 Julai 2020

Shirika la Amnesty International limesema serikali lazima zibebeshwe dhamana kwa vifo vya wahudumu wa afya vinavyotokana na ugonjwa wa Covid 19 kwa kushindwa kuwawekea mazingira mazuri na salama ya kazi.

https://p.dw.com/p/3fEqH
Bangladesh | Coronavirus-Pandemie | Beximco-Mitarbeiter in Savar
Picha: AFP/M. U. Zaman

Amnesty International imetoa ripoti mpya inayoeleza madhila wanayopitia wahudumu wa afya duniani kote wakati huu wa janga la virusi vya Corona.

Kwa mujibu wa takwimu za Amnesty International, ni kuwa zaidi ya wahudumu wa afya 3000 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid 19 duniani kote, idadi hiyo ikitajwa kuwa huenda ikawa chini zaidi tofauti na idadi halisi.

Katika hali ya kutia wasiwasi zaidi, Amnesty International imenakili visa vya baadhi vya wahudumu wa afya waliotishiwa maisha, waliokamatwa au hata kufutwa kazi baada ya kutoa malalamishi kuhusu mazingira mabaya ya kazi na usalama wao wanapokuwa kazini.

Fiebermessen bei Passanten in Sao Paulo, Brasilein
Wananchi wakipimwa joto kabla ya kuingia madukani huko Sao PauloPicha: Reuters/A. Perobelli

Mtafiti na mshauri kuhusu haki za uchumi, jamii na utamaduni katika shirika hilo Sanhita Ambast amesema kwamba, "Wakati maambukizi ya virusi vya Corona yanaendelea kuenea kwa kasi duniani, tunazitolea wito serikali kulichukulia kwa uzito suala la afya na usalama wa wahudumu wa afya. Serikali hazifai kurudia makosa ya baadhi ya serikali zilizokosa kulinda haki za wahudumu wa afya kwani huenda kukawa na athari mbaya.”

Kwa wakati huu hakuna utaratibu maalum uliowekwa wa kufuatilia ili kujua idadi kamili ya wahudumu wa afya waliofariki kutokana na ugonjwa wa Covid 19. Hata hivyo, Amnesty International imekusanya data kutoka sehemu mbalimbali zinazoonyesha kuwa zaidi ya wahudumu wa afya 3000 wamefariki kutokana na ugonjwa huo wa mapafu katika nchi 79 duniani kote.

Nchi zenye vifo vingi vya wahudumu wa afya

Nchi zilizorekodi idadi kubwa ya vifo vya wahudumu wa afya duniani ni Marekani yenye vifo 507, Urusi yenye vifo 545, Uingereza yenye vifo 540, Brazil yenye vifo 351, Mexico yenye vifo 248, Italia yenye vifo 188, Misri yenye vifo 111, Iran yenye vifo 91, Ecuador ina vifo 82 ilhali Uhispania imerekodi vifo 63 vya wahudumu wa afya.

Ägypten I Coronavirus
Wahudumu afya nchini Misri wamevalia mavazi ya kujikinga wakati wakiwapima watuPicha: picture-alliance/AP/N. El-Mofty

Hata hivyo, idadi hiyo ya vifo huenda ikawa ni ndogo tofauti na hali halisi kwani kupata takwimu kamili na sahihi imekuwa ni vigumu. Kwa mfano takwimu zilizotolewa na vyama vya madaktari na wahudumu wa afya nchini Misri na Urusi zimepingwa na serikali zao. Vile vile, Ufaransa imekusanya data zake kutoka kwa baadhi ya hospitali na vituo vya afya.

Mifano hii ikionyesha wazi kuwa idadi ya vifo vya wahudumu wa afya vinavyotokana na ugonjwa Covid 19 huenda ikawa juu zaidi ya inavyoripotiwa.

Amnesty International imeongeza kuwa wahudumu wa afya wamelalamika kuhusu uhaba wa vifaa kinga katika takriban nchi zote 63 zilizofanyiwa utafiti na shirika hilo.

Pia, marufuku ya biashara kati ya nchi na nchi imechangia kuongezeka kwa tatizo hili la uhaba wa vifaa kinga. Mnamo mwezi Juni mwaka 2020, nchi 56 pamoja na Umoja wa Ulaya ziliweka marufuku ya usafirishaji wa baadhi vya vifaa kinga.