1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AMMAN: Umoja wa Ulaya wayalaani mashambulio ya mabomu nchini Jordan

10 Novemba 2005
https://p.dw.com/p/CEJp

Umoja wa Ulaya umeyalaani mashambulio matatu ya kigaidi yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 57 katika mji mkuu wa Jordan, Amman.

Waziri wa mambo ya kigeni wa umoja huo, Javier Solana, amesema mashambulio hayo hayawezi kukubalika. Solana ametuma risala za rambirambi kwa mfalme wa Jordan, Abdula wa pili, ambaye ameyaeleza mshambulio hayo kuwa ya kigaidi.

Bwana Solana anatarajiwa kuitembelea mashariki ya kati juma lijalo, ikiwa ni pamoja na Jordan, kuziongezea nguvu juhudi za kutafuta amani kati ya Israel na Palestina.

Miripuko hiyo iliyotokea katika hoteli za Hyatt, Radisson na Days Inn, ilisababisha watu wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa.

Kundi la al-Qaeda nchini Irak, linaloongozwa na Abu Musab al-Zarqawi, limedai limeyafanya mashambulio hayo.

Japan na Uingereza zimeyalaani pia mashambulio hayo zikisema ugaidi hauwezi kukubalika kwa njia yoyote ile. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Japan amesema nchi hiyo inapinga matendo hayo ya kinyama yaliyowaua na kuwaumiza watu wasio na hatia.