1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Sadr aonyesha nguvu yake kwa mara nyengine Irak

5 Agosti 2022

Mamia kwa maelfu ya Wairaki wameitikia mwito wa kiongozi wa kidini wa Kishia mwenye ushawishi mkubwa Muqtada al-Sadr na kukusanyika kwa maombi katika eneo lililo na ulinzi mkali lenye afisi za serikali Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4FB7R
Iraq Protests
Picha: Nabil al-Jurani/AP/picture alliance

Mkusanyiko huo umefanyika huku mgogoro wa kisiasa unaotishia kuiangusha Baghdad ukizidi.

Mkusanyiko huo kwa sala ya Ijumaa umeonyesha kwa mara nyengine nguvu aliyo nayo Al-Sadr, ambaye nguvu zake za kisiasa zinatokana na ufuasi mkubwa alio nao mashinani.

Alikuwa ametoa wito kwa wafuasi wake kutoka kote nchini Irak kujitokeza na kusalia katika eneo hilo lililo na majengo ya serikali na balozi za nchi za kigeni.

Alishinda uchaguzi akashindwa kuunda serikali

Wafuasi hao waliwasili na kusimama nje ya eneo hilo licha ya jua kali lililokuwa linapiga huku nyuzi joto zikifikia 48 katika vipimo vya celsius. Baadhi ya watu wanaripotiwa kuwa walizirai na wakakimbizwa hospitali, baada ya kusubiri kwa muda mrefu kwa sala kuanza.

Wafuasi hao walisimama wakiutazama mnara wa ushindi, uliowekwa katika kipindi cha utawala wa Saddam Hussein ili kuadhimisha vita vya Iran na Irak. Mnara huo ulijengwa kwa ajili ya kufanya magwaride ya kijeshi.

Proteste in Irak
Wafuasi wa al-Sadr wakielekea katika eneo lenye majengo ya serikaliPicha: Ahmed Saad/Reuters

Wakati huo huo, mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa kwa Irak Jeanine Hennis-Plaschaert, amesema amekutana na Al-Sadr katika mji mtakatifu wa kusini wa Najaf leo. Baada ya mkutano huo amewaambia waandishi wa habari kwamba wamezungumza umuhimu wa kupata suluhu kwa mgogoro wa kisiasa uliopo.

Al-Sadr ndiye aliyekuwa mshindi mkuu katika uchaguzi uliofanyika Oktoba ila alishindwa kuunda serikali isiyokuwa na vyama vyenye usuhuba na Iran kama alivyokuwa ameahidi. Aliwalazimisha wabunge wake kuachia ngazi bungeni na kwa sasa analizuia bunge kuchagua serikali mpya na anaitisha uchaguzi wa mapema.

Kiongozi huyo maarufu ana mamilioni ya wafuasi na ameonyesha mara kadha kwamba anaweza kuweka shinikizo la kisiasa kwa kuwaita maelfu ya hao wafuasi wake ambao sehemu kubwa ni Waislamu wa Kishia.

Viongozi wenzake wa Kishia ndio mahasimu wake wakuu

Babake Al-Sadr, Mohammed Sadiq al-Sadr, aliuwawa na serikali ya Saddam Hussein kutokana na kumpinga waziwazi kiongozi huyo wa zamani wa kiimla. Sadr baadae aliwarithi wafuasi wa babake na baada ya uvamizi wa Marekani nchini Irak kupelekea kuangushwa kwa utawala wa Saddam Hussein, al-Sadr alianza mapambano na majeshi ya Marekani.

Proteste in Irak
Wafuasi wa Al-sadr walipolivamia bungePicha: Thaier Al-Sudani/Reuters

Mahasimu wake lakini ni viongozi wenzake wa Kishia na vyama vinavyoegemea upande wa Iran kwa kuwa Sadr mwenyewe amejiweka kama mzalendo ambaye anakataa katakata uingiliaji wa mataifa ya kigeni.

Hao mahasimu wake, kama vile yeye mwenyewe, wanaungw amkono na wanamgambo waliojihami kwa silaha nzito ila hawana ushawishi mkubwa kama alivyo nao yeye kwa wafuasi wake kindakindaki.

Chanzo: Reuters/AP