1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Bashir alainisha matamshi yake dhidi ya waandamanaji

7 Februari 2019

Rais wa Sudan Omar al-Bashir amesema siku ya Jumatano kuwa sheria kandamizi inayozozaniwa pamoja na hali ngumu ya uchumi ndiyo vimechochea hasira miongoni mwa vijana wanaoongoza maandamano ya kumtaka aachie madaraka.

https://p.dw.com/p/3Ctzv
Suadan Präsident Omar Al Bashir
Picha: Reuters/M. Abdallah

Matamshi hayo ya al Bashir anayekabiliwa na maandamano ya kila uchao dhidi ya utawala wake yameonesha mabadiliko makubwa ya matamshi ya kiongozi huyo kuelekea waandamanaji ambao katika siku za karibuni aliwafananisha na panya.

Akizungumza na waandishi wa habari walioalikwa katika Ikulu ya rais mjini Khartoum al-Bashir amekiri kwa mara ya kwanza kuwa sehemu kubwa ya waandamanaji ni vijana waliovunjwa moyo na hali ya uchumi ikiwemo mfumuko wa bei uliopandisha gharama za vyakula na ukosefu wa ajira.

Maandamano ambayo yalianza Dec 19 mwaka uliopita yalichochewa na kupanda kwa bei za vyakula, ukosefu wa fedha za kutosha kwenye mabenki na matatizo mengine ya kiuchumi lakini tangu hapo yamegeukia utawala wa miaka 30 wa rais al-Bashir

Polisi imekuwa ikitumia gesi ya kutoa machozi na katika baadhi ya matukio risasi za moto kujaribu kuyasambaratisha maandamano hayo.

Kauli hiyo ya Bashir yenye ishara ya kusaka maridhiano ni tofauti kabisa na ile aliyoitoa hapo kabla alipowafananisha waandamanji kuwa sawa na panya wanaopaswa kurejea kwenye mashimo yao na inatoa tafsiri kuwa ni sehemu ya mkakati mpya wa kupunguza ghadabu za wanaompinga.

Waandishi habari kuachiwa huru

Sudan Khartum Anhänger  Sadiq al-Mahdi  Opposition
Picha: Reuters/M. Nureldin Abdallah

Pia, katika hali isiyotarajiwa, al-Bashir alikwenda mbali zaidi na kutoa ahadi ya kuwachilia huru waandishi wa habari wanaoshikiliwa na utawala wake.

Bashir amesema waandishi wote wa habari ambao wamekamatwa na kufungwa kuhusiana na ghasia za maandmanao wataachiwa hruu. Inakisiwa idadi ya waandhsi wa habari walio jela inafikia 16.

Wakati wa mkutano huo wa Jumatano al-Bashir alionya dhidi ya kuvuruga uthabiti wa taifa hilo akitolea mfano wa hali ya mambo nchini Libya ambayo imekuwa katika machafuko makubwa ya kisiasa tangu mwaka 2011 baada ya kuzuka mapigano yaliyouangusha utawala wa Muammmar Ghadaffi.

Watetezi wa haki za binadamu wamesema kiasi watu 45 wameuawa tangu mandamano hayo yalipoanza lakini serikali imesema idadi waliopoteza maisha ni 30 ikiwemo maafisa wawili wa polisi.

Wanaharakati wa kisiasa, wajumbe wa asasi za kiraia na waandishi wa habari wamekuwa wakikamtwa na kuwekwa kizuizini.

Sheria kandamizi kichocheo kingine cha maandamano

Sudan Khartum Proteste gegen Präsident Al-Baschir
Picha: Reuters/M.N. Abdallah

Rais al-Bashir aligusia pia utekelezaji wa sheria tata za kusimamia utulivu wa umma kuwa chanzo kingine kilichochochea hasira miongoni mwa waandamanaji vijana. 

Kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu sheria hizo zinakiuka kwa sehemu kubwa haki za wanawake ikiwemo marufuku ya uvaaji suruali kwa wanawake..

Adhabu kali ikiwemo faini na kutumikia kifungo jela zimekuwa zikitolewa kwa wanawake wanaozivunja.

Makundi hayo yamesema chini ya sheria hizo zaidi ya wanawake 15,000 walihukumiwa adhabu ya kucharazwa viboko mnamo 2016.

Wakati huo huo hapo jana al Bashir aliendeleza lawama zake kwa Marekani kwa kuwa chanzo cha kudorora kwa uchumi wa nchi yake kutokana na vikwazo vya kibiashara ilivyowekewa na nchi hiyo mwaka 1997   

Licha ya vikwazo hivyo kuondolewa Oktoba 2017 lakini havijasaidia pakubwa katika kuimarika kwa hali ya uchumi nchini humo.

Marekani bado imeiorodhesha Sudan kuwa taifa linalofadhili ugaidi katika orodha inayozijumuisha pia Iran, Syria na Korea kaskazini.

Mwandishi: Rashid Chilumba/Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga