1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajira kwa watoto yaongezeka ulimwenguni

10 Juni 2021

Umoja wa Mataifa umesema ulimwengu kwa mara ya kwanza umeshuhudia ongezeko la idadi ya watoto wanaofanyishwa kazi katika kipindi cha miongo miwili. Idadi ya watoto wanaotumikishwa ilifikia milioni 160 mwanzoni mwa 2020

https://p.dw.com/p/3ufx3
Mosambik | Provinz Zambezia | Handwerklicher Edelsteinabbau
Picha: Roberto Paquete/DW

Katika ripoti ya pamoja, Shirika la Kazi la Kimataifa – ILO na lile la Umoja wa Mataifa UNICEF, yamesema idadi ya watoto wanaotumikishwa ilifikia milioni 160 mwanzoni mwa mwaka wa 2020 -- ikiwa ni ni ongezeko la watoto milioni 8.4 katika miaka minne.

Kuongezeka huko kulianza kabla ya kuzuka janga la corona na  kunaonyesha mabadiliko makubwa ya muenendo ambao ulikuwa umeshuhudia idadi ya ajira kwa watoto ikipungua kwa milioni 94 kati ya mwaka wa 2000 na 2016.

Ripoti hiyo imesema wakati mgogoro wa COVID-19 ulianza kushika kasi, karibu mmoja kati ya watoto 10 ulimwenguni afanyishwa kazi, huku eneo la kusini mwa jangwa la Sahara likiathirika pakubwa. Hii ni kutokana na ongezeko la idadi ya watu, migogoro na umaskini.

 Liberia leeres Klassenzimmer einer Schule in Monrovia
Kufungwa shule kulichangia zaidi ajira kwa watotoPicha: picture-alliance/dpa/A. Jallanzo

Hatua za haraka zahitajika

Mkuu wa shirika la UNICEF Henrietta Fore amewaambia waandishi wa habari kuwa ulimwengu unabaki nyuma katika vita vya kukomesha ajira kwa watoto "Familia ziko katika hali ngumu na zinageukia ajira kwa watoto kama uamuzi wa mwisho. Lazima tukatae hilo.

Tunazihimiza nchi kutanua hatua za msaada wa kipato kama vile mafao kwa watoto ili kuwarudisha watoto shuleni wanakostahili kuwa, na kuwekeza katika mipango ya kuwalinda na kuwazuia kutumiwa." Amesema Fore.

Mashirika ya ILO na UNICEF yameonya kuwa kama hatua ya dharura haitochukuliwa kusaidia idadi inayopindukia ya familia kutumbukia katika umaskini, karibu watoto milioni 50 zaidi huenda wakalazimishwa kufanya kazi katika miaka miwili ijayo. Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder anasema takwimu hizi mpya zinatuma onyo kubwa. "Hatari ni kuwa, kutokana na hili janga na lilichokifanya katika ulimwengu wa ajira, na tunajua lilichokifanya; limeharibu ajira nyingi, limepunguza mapato ya ajira, na limewatumbukiza watu katika umaskini na mazingira magumu kabisa." Amesema Ryder

Ripoti hiyo inayochapishwa kila baada ya miaka minne, inaonyesha kuwa Watoto wa chini ya umri wa miaka mitano na 11 ni sehemu ya zaidi ya nusu ya idadi ya jumla ulimwenguni.

Wavulana wana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa, wakiwa sehemu ya watoto milioni 97 kati ya 160 wanaofanyishwa kazi mwanzoni mwa mwaka wa 2020.

AFP/Reuters