1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAfrika

Afrika yaitaka Marekani kurefusha mkataba wa AGOA

Hawa Bihoga
2 Novemba 2023

Umoja wa Afrika unataka Marekani irefushe Mpango wake wa biashara wa AGOA kwa angalau miaka 10, wakati ambapo baadhi ya wabunge wa Marekani wakitaka nchi hiyo nayo kunufaika katika mpango barani Afrika.

https://p.dw.com/p/4YL0j
Waziri wa mambo ya Nje Marekani Antony Blinken akiwa na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Waziri wa mambo ya Nje Marekani Antony Blinken akiwa na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Picha: Andrew Harnik/AFP

Mataifa takriban 40, kutoka kusini mwa jangwa la Sahara ambayo yananufaika na mpango wa Marekani wa fursa za ukuaji wa kiuchumi unajulikana kama AGOA, watafanya mazungumzo na wajumbe wa Marekani kwa siku tatu mjini Johannesburg.

Joy Basu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika anasema, kuichagua Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni ishara ya wazi kwamba wamejidhatiti katika kuimarisha mahusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Afrika Albert Muchanga amesema Afrika inataka Bunge la Marekani la Congress kurefusha mpango huo wa biashara angalau kwa kipindi cha miaka 10 na endapo kutakuwa na mabadiliko ya aina yoyote yatajadiliwa kwa siku za usoni.

"Kurefushwa kwa miaka 10 hadi 20 ni kutoa hakikisho kwa jumuia ya wawekezaji," Muchanga aliwaambia mawaziri na maafisa wa Marekani waliohudhuria mkutano huo.

Soma pia:Nchi za Kiafrika hazitumii nafasi ya mkataba wa AGOA

Alisema endapo Marekani itaamua kinyume na hapo kunaweza kutatiza uwekezaji baina ya pande hizo mbili.

Kamishna huyo aliongeza kwamba , Marekani haitapata msamaha wa kikodi katika eneo jipya la biashara huria barani Afrika.

Ameitoa kauli hiyo wakati baadhi ya wabunge wa Marekani wanataka mpango huo uwe na usawa kwa pande zote.

Marekani itarefusha mpango wa AGOA?

Mpango huo ambao unatajwa kuyanufaisha mataifa ya Afrika unatarajiwa kumaliza muda wake mnamo Septemba 2025, na kwa sasa majadiliano yanaendelea ili uweze kurefushwa na kuboreshwa.

Viongozi wa mataifa ya Afrika wakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Viongozi wa mataifa ya Afrika wakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Wabunge wa Marekani pamoja na utawala wa Rais Joe Biden wanaunga mkono kurefushwa na kuundwa upyakwa mpango wa AGOA ambao ulishuhudia mauzo ya nje ya Afrika yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 10 yakiingia Marekani bila kutozwa ushuru  mwaka jana.

Afisa wa biashara wa ngazi za juu katika utawala wa Biden Constance Hamilton alisema juma lililopita kwamba, Congress inapaswa kuzingatia mabadiliko ambayo "yatafanya mpango huo kuwa na matokeo chanya zaidi".

Serikali za Afrika na baadhi ya makundi katika sekta ya viwanda nchini Marekani yanaonya kwamba marekebisho yoyote kama sehemu katika kuongezea muda mpango huo yanaweza kuchelewesha uidhinishwaji wake.

Soma pia:Marekani yataka kuurefusha mkataba wa AGOA

Hata hivyo Muchangwa amesema iwapo kuna maboresho yoyote yafanyike ikiwa tayari muda umekwisha ongezwa. 

Walter Ngumo Mchambuzi wa masuala ya uchumi nchini Tanzania anasema pande zote zitashuhudia makali ya kiuchumi ikiwa mpango huo utacheleweshwa.

"Msamaha wa kodi ulisaidia Afrika kufanya biashara Marekani, endapo utacheleshwa utatatiza pande zote" Ngumo aliiambia DW 

Kipimo cha demokrasia chayaengua mataifa

Bunge la Marekani, Congress, mnamo mwaka 2000 liliidhinisha Mpango wa AGOA kama msingi wa sera ya uchumi kati ya Marekani na bara la Afrika.

Mpango huo ukitoa fursa ya kutotozwa kodi nchini Marekani kwa nchi ambazo zimeridhia mpango huo kwa kutimiza vigezo vya kidemocrasia ambavyo hutathminiwa kila mwaka.

Mwishoni mwa mwezi uliopita Marekani ilitangaza kusitisha ushiriki katika mpango wa AGOA kwa mataifa ya Gabon, Niger, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati, kutokana na serikali za mataifa hayo kushindwa katika masuala ya utawala bora na Haki za binadamu.

Museveni aitetea sheria ya kupinga ushoga

Uganda ilikosoa hatua hiyo ya Marekani ya kuiondoa na nchi nyingine za Afrika katika mpango huo, ikisema hatua hiyo ni kuadhibu nchi ambazo zinapinga kuwekwa kwa maadili ambayo hayaendani na Afrika.

Soma pia:Ethiopia yasikitishwa kwa kuondolewa katika mpango wa AGOA

Odrek Rwabwogo, mshauri maalum wa rais Yoweri Museveni, alisema mapango wa AGOA unalengo la kukuza uchumi wa Afrika na si kuadhibu mataifa.

"Haikuanzishwa kama fimbo ya kuwaathibu wa Afrika, lakini hivi ndivyo inatumika kwa sasa." Alisema Rwabwogo katika taarifa yake.

Afrika iko mbioni kuanzisha eneo jipya la biashara huria katika bara zima, linalojulikana kama AfCFTA, ambalo linalenga kuwaleta pamoja watu bilioni 1.3 katika ukanda wa kiuchumi wenye thamani ya dola trilioni 3.4.