1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Mashariki yakubaliana na UN kuhusu wakimbizi

18 Aprili 2023

Jumuiya ya Afrika Mashariki na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, zimetia saini mkataba wa makubaliano, wenye lengo la kuhuisha na kuimarisha ushirikiano katika kushughulikia masuala ya wakimbizi

https://p.dw.com/p/4QF0d
Tansania Burundis Flüchtlinge
Picha: Tchandrou Nitaga/AFP/Getty Images

Jumuiya ya Afrika Mashariki na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, zimetia saini mkataba wa makubaliano, wenye lengo la kuhuisha na kuimarisha ushirikiano katika kushughulikia masuala ya wakimbizi na waomba hifadhi pamoja na kuhitaji ulinzi wa kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Makubaliano hayo yaliyofikiwa katika ofisi za makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki Arusha Tanzania, pamoja na mambo mengine yamelenga kulinda haki za wakimbizi na wanaotafuta hifadhi.

Mkataba huo pia, umelenga kuziunga mkono nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu wakimbizi, ikiwa ni pamoja na kuwarudisha makwao kwa hiari.

Sera ya usimamizi wa wakimbizi ya jumuiya ya Afrika Mashariki tayari imeandaliwa na kuafikiwa na nchi wanachama, ambapo hatua inayofuata ni kuhakikiwa na kupitishwa na baraza la kisekta, kabla ya kupitishwa na baraza la mawaziri kwa mujibu wa sheria za jumuiya hiyo.