1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini: Wabunge wa upinzani wavuruga hotuba ya rais

Daniel Gakuba
14 Februari 2020

Wabunge wa chama cha Economic Freedom Fighters, EFF cha mwanasiasa machachari wa Afrika Kusini, Julius Malema, wamefanya fujo na kumlazimisha rais Cyril Ramaphosa kuchelewesha hotuba yake ya mwaka kuhusu hali ya nchi.

https://p.dw.com/p/3Xmji
Südafrika - Wahl / Vorsitzender der Partei für wirtschaftliche Freiheitskämpfer (EFF), Julius Malema
Julius Malema na wabunge wenzake wa chama cha EFF (picha ya maktaba).Picha: picture-alliance/M. Safodien

Wabunge wa chama cha Economic Freedom Fighters, EFF kinachoongozwa na mwanasiasa machachari wa Afrika Kusini, Julius Malema, wamefanya fujo bunge na kumlazimisha rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa kuchelewesha hotuba yake ya mwaka kuhusu hali ya nchi.

Katika fujo hizo zilizodumu kwa takribani saa nzima, Malema na wenzake walikuwa wakipinga kuwepo bungeni kwa rais wa mwisho wa enzi za utawala wa kibaguzi, Apartheid F.W. De Klerk, wakisema amekaidi kujutia madhambi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi.

''Tunaye muuaji katika jengo hili, tunaye ndani ya nyumba hii, mtu ambaye mikoni yake imejaa damu ya watu wasio na hatia,'' amesema kwa sauti kubwa Malema wakati ambapo Rais Ramaphosa alitakiwa kuanza kutoa hotuba yake.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa
Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika KusiniPicha: Reuters/R. Bosch

Spika wa bunge Thandi Modise ameahirisha kwa muda kikao hicho cha bunge kutokana na ghasia hizo, akimwambia Malema na wenzake kuwa ''kutumia uhuru wenu wa kutoa mawazo kwa kukanyaga haki za wengine, hiyo ni vurugu.''

Nishati endelevu kama chachu ya ukuaji wa uchumi

Ni utaratibu uliozoeleka nchini Afrika Kusini, kuwa marais wa zamani huwepo bungeni wakati rais aliyeko madarakani anapowasilisha hotuba yake ya mwaka.

Katika hotuba yake baada ya vurugu hizo kutulia, Rais Ramaphosa amesema Afrika Kusini itaanza hivi karibuni kuzalisha nishati endelevu ya ziada kupambana na upungufu wa umeme unaoikumba nchi hiyo.

Ameahidi pia kuanzisha hatua mbali mbali za kuimarisha sekta ya uchumi na fedha, zikiwemo kuunda fuko la kitaifa kwa ajili ya kulinda raslimali za nchi, na benki ya kitaifa itakayosaidia kufikisha hudumu za kifedha kwa watu wengi zaidi.

Ramaphosa aliingia madarakani kwa ahadi ya kuufufua uchumi wa Afrika Kusini na kurejesha nidhamu uongozini, baada ya utawala wa mtangulizi wake Jacob Zuma ulioandamwa na kashfa na tuhuma za rushwa.

 

afpe, rtre