1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika kuongoza kwa kilimo cha bangi ya matibabu

25 Novemba 2019

Kundi la wanasayansi, watafiti na wajasiriamali limesema bara la Afrika linaweza kufikia kuwa mzalishaji mkubwa wa bangi inayotumika kwa ajili ya matibabu.

https://p.dw.com/p/3TgxX
Hanfanbau
Picha: Imago Images/Chromorange

Jordan Curl; mtaalamu kutoka Kituo cha Uwekezaji na Utafiti wa Bangi cha nchini Israel amewaambia wajumbe wanaohudhuria mkutano wa teknolojia ya mihadarati mjini Cape Town, Afrika ya Kusini, kuwa "Afrika itakuwa kitovu cha uzalishaji bangi duniani."

Kulingana na taasisi moja ya mjini London, soko la bangi na bidhaa za zao hilo kutoka Afrika linatarajiwa kufikia thamani ya dola bilioni 7.1 ifikapo mwaka 2023.

Wawekezaji wengi wanavutiwa kuwekeza kwenye kilimo cha mihadarati hiyo kusini mwa Afrika kutokana na uwepo wa ardhi kubwa, idadi ya kutosha ya wafanyakazi wanaoweza kuajiriwa kwa fedha chache na hali nzuri ya hewa inayowezesha kustawi kwa bangi.

Afrika Kusini ndiyo taifa linaloongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa bangi likifuatiwa na Zimbabwe na Lesotho, ambazo hivi karibuni zimetoa leseni ya kilimo cha bangi kwa matumizi ya kitabibu.