1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika kufungua anga huku corona ikizidi kusambaa

6 Julai 2020

Wakati visa vya maambukizi ya maradhi ya COVID-19 vikizidi kuongezeka katika maeneo mengi ulimwenguni, bara la Afrika linakabiliwa na ugumu katika kuamua kuhusu iwapo mataifa yaruhusu ndege za kimataifa.

https://p.dw.com/p/3eqdt
Ethiopian Air Lines
Picha: Ethiopian Air Lines

Wakati visa vikizidi kuongezeka ulimwenguni, kisiwani cha Seychelles kilikuwa salama kabisa. Kwa siku 70 mfululizo hakukua na kisa chochote na hatimaye ndege mbili zikaingia nchini humo zikiwa na abiria zaidi ya 200, na miongoni mwao walikuwa wameambukizwa virusi vya corona. Taifa hilo hatimaye likaripoti visa 11 vilivyoongezeka kwa kasi hadi 81 kati ya Juni 24 na 30.

Sasa Seychelles, kisiwa kilichopo katika bahari ya Hindi kimesogeza mbele muda wa kurejesha safari za ndege za kibiashara kuingia nchini humo hadi Agosti 1 iwapo tu hali itakuwa nzuri.

Mataifa ya Afrika yanakabiliwa na ugumu katika kufanya maamuzi ya ama kuziruhusu tena ndege za kimataifa kuingia kwenye mataifa hayo ambayo mengi yana mifumo dhaifu za kiafya na mengine yakihofu kuzorota zaidi kwa chumi zao katika wakati ambapo maambukizi nayo yanaongezeka kwa kasi.

Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika, Matshidiso Moeti aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi iliyopita siku moja baada ya Misri kufungua tena safari za ndege mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miezi mitatu kuwa hiki ni kipindi tete mno.

Mataifa mengine yanajiandaa kufuata mkondo huo hata katika wakati ambapo Afrika ina visa zaidi ya 463,000 vilivyothibitishwa hadi Jumapili iliyopita vya virusi vya corona na Afrika Kusini, ambayo ina uchumi mkubwa zaidi barani humo, ikiwa inapambana na kuwatibu wagonjwa wa COVID-19.

Süfafrika Johannesburg | Covid-19 Impfstoff Tests beginnen
Mmoja ya wakazi wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini akipata chanjo ya majaribio ya COVID-19.Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Sibeko

Kulingana na Umoja wa Afrika, tayari bara hilo linakabiliwa na mdororo wa uchumi wa robo ya karne na limekwishapoteza karibu dola bilioni 55 katika sekta zake za utalii na usafirishaji katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Usafiri wa anga pekee umepoteza kiasi dola bilioni 8.

Mataifa mengi barani humo yalifunga anga ili kukabiliana na kusambaa janga hilo la COVID-19. Kulingana na mkuu wa WHO Dr. Tedros Adhanom Gebreyesus wakuu wengi wa mataifa ya Afrika sasa wameonyesha nia ya kurejesha safari hizo.

Wiki iliyopita, idadi ya safari za kimataifa ilipanda kwa kiasi kikubwa. Kati ya Juni 30 na Julai 2 safari za ndege za kila siku ziliongezeka kutoka 3,960 hadi 6,508.

Senegal itarejesha safari zake kuanzia Julai 15 na Jumuiya ya kiuchumi kwa mataifa ya Magharibi, ECOWAS inataraji kufungua tena anga Julai 21. Nigeria itarejesha safari za ndani Julai 8 na Rwanda, Agosti 1.

WHO inayasisitiza mataifa hayo kuzingatia uwezo wao wa kukabiliana na visa vipya iwapo vitaingizwa kupitia safari hizo. Viongozi wa kikanda wa baraza la kimataifa la usafirishaji wa anga katika barua yao ya wazi kwa mawaziri wa Umoja wa Afrika walisema wao wako tayari.

Afrika ilishuhudia safari chache zaidi za anga katika kipindi cha janga la corona ikilinganishwa na kanda nyingine ulimwenguni. 

Sikiliza Zaidi:

Vita dhidi ya COVID -19 Afrika Mashariki

Chanzo: AFPE.