1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

23 Agosti 2024

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na kuendelea kusambaa kwa kwa virusi vya homa ya nyani barani Afrika, maandamano ya Wamasai katika hifadhi ya Ngorongoro Tanzania nayo yameangaziwa.

https://p.dw.com/p/4jpyC
Magazeti ya Ujerumani
Magazeti ya UjerumaniPicha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Der Tagesspiegel

Der Tagesspiegel liliandika, virusi vinavyosababisha ugonjwa huo vinaendelea kusambaa kwa kasi katika mataifa kadhaa barani humo. Kulingana na taarifa zilizochapishwa na mamlaka ya afya ya Umoja wa Afrika CDC kwa juma lililopita pekee, visa vipya 1,200 vilivyothibitishwa au kutiliwa shaka vilivyotokana na aina tofauti za virusi vya homa ya nyani viligunduliwa.

Der Tages spiegel limeandika, Ugonjwa huo unaweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama, na hata kwa binadamu hasa kwa njia ya kujamiiana. Wataalamu wana wasiwasi hasa na aina ya kirusi kinachosababisha ugonjwa huo cha 1b kilichosambaa kwa kiasi kikubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na baadhi ya nchi za Kiafrika.

Kuhusu ugonjwa huo huo uliotangazwa na Shirika la Afya duniani kuwa dharura ya afya ya Umma, gazeti la Welt Online lenyewe limeandika, homa ya nyani inahitaji juhudi za pamoja  si tu barani Afrika. Zaidi gazeti hilo linaeleza kuwa, wataalamu wanahofu kuwa maradhi hayo yanaweza kusambaa zaidi Ulaya.

 Zeit Online

 Zeit Online wiki hii liliyaangazia maandamano ya Wamasai katika hifadhi ya Ngorongoro nchini Tanzania . Zaidi gazeti hilo la mtandaoni limefafanua kuwa, maelfu ya watalii hufika katika eneo hilo ambalo ni moja ya vivutio vya kipekee duniani wakati  wakaazi asilia wa eneo hilo wakishindwa kunufaika. Na sasa wameambua kupambana.

Mamia ya wakaazi hao ambao ni jamii ya wamasai walizuwia barabara inayoiunganisha hifadhi hiyo ya Ngorongoro na mbuga jirani ya wanyama ya Serengeti.

Maandamano ya Wamasai Ngorongoro
Waandamanaji wa jamii ya Wamasai katika hifadhi ya NgorongoroPicha: DW

Badala ya watalii  kuendelea na safari zao, magari yaliyowabeba yalijikuta katikati ya wanaume, wanawake na watoto waliovalia nguo za asili wakiwa wameshikilia mabango ambayo baadhi yalisomeka, "ardhi yetu, maisha yetu", na mengine yaliandikwa: " Wafungwa wanaruhusiwa kupiga kura Tanzania. Wamasai hawaruhusiwi hata kujiandikisha kupiga kura".  Katika maandamano hayo walizungumzia kutengwa na kuondolewa kwa nguvu kwenye ardhi yao.

Gazeti hilo limemnukuu mwanasheria na msemaji wa Jamii ya wamasai Joseph Oleshangay aliyesema kuwa serikali ya Tanzania inawataka Wamasai waondoke kwenye hifadhi hiyo ya Ngorongoro. Hivyo imewanyima wakaazi hao huduma za afya, elimu na sasa wamenyimwa pia hata haki ya kupiga kura . Na huo ndiyo mzizi wa maandamano hayo.

Süddeutsche Zeitung

Süddeutsche Zeitung liliangazia kupungua kwa kiasi kikubwa kwa idadi ya wahamiaji wanaopitia Afrika ya Kaskazini kuingia Italia. Kwa miaka mingi, wahamiaji wanaovuka kupitia bahari ya Mediterania, operesheni za uokoaji baharini na vituo vya hamiaji vilivyosheheni watu kuliko uwezo wao zilikuwa mada za kila wakati kwenye vyombo vya habari .

Kwa sasa mada hizo hazisikiki tena kama awali. Hii ni kwa sababu idadi ya boti zinazowabeba wakimbizi imepungua kwa kasi kubwa, kulingana na wizara ya mambo ya ndani ya Italia. Kwa mwaka huu pekee ni wahamiaji 38,000 pekee waliowasili Roma ikilinganishwa na  mwaka uliopita muda kama huu ambapo wahamiaji 105,000 walifika Italia kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kipindi cha nyuma, wahamiaji wengi walitokea Tunisia, lakini sasa Libya ndiyo kituo kikuu cha wahamiaji kuondokea. Licha ya kuwa kuna wakimbizi wengi na wahamiaji duniani kuliko awali, idadi ya wanaokimbilia Ulaya imepungua.

Hii ni kwa sababu, Umoja wa Ulaya na Italia ziliingia makubaliano na Tunisia pamoja na Libya. Nchi hizo mbili za Afrika zilipewa fedha ili kuwazuwia wahamiaji kuingia Ulaya. Mwaka 2023 Umoja wa Ulaya uliiahidi Tunisia Euro milioni 105 na sasa Italia na Ufaransa zinataka kuzipatia fedha nyingi zaidi.

Pamoja na mafanikio hayo ya kuwadhibiti wahamiaji, watetezi wa haki za binadamu na ripoti za waandishi wa habari zinasasema kuwa haki za wakimbizi zinakiukwa Tunisia. Walinzi wa Pwani wanatuhumiwa kwa kuwanyanyasa na kuwafanyia ukatili

Kwa upande wa Libya hali pia si nzuri. Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti iliyoeleza kuwa wahamiaji 29 walikufa katika jangwa na pia katika eneo la mpakani, kuligunduliwa kaburi la pamoja walimozikwa wahamiaji 65

die tageszeitung

die tageszeitung liliimulika habari njema kuhusu misaada ya chakula ilivyofanikiwa kufika Darfur. Baada ya kufungwa kwa muda mrefu na serikali ya kijeshi ya Sudan, kwa mara ya kwanza mpaka wa Adre ulifunguliwa na kuuruhusu msafara wa mpango wa chakula wa Umoja wa Mataifa kupitisha misaada. Mpaka huo ni kivuko kikubwa na muhimu kati ya Chad na Sudan. Kwa mara ya mwisho kilitumiwa na shirika hilo la chakula  mwezi Machi mwaka huu.

Darfur El Fasher
Picha: AFP

Zaidi ya malori 131 ya msaada huo ya chakula yaliripotiwa kuwepo mpakani. Afisa wa shirika la mpango wa chakula WFP  nchin Sudan Rania Dagash, alithibitisha Jumatano kuwa tayari malori kadhaa yalishavuka mpaka.

die tageszeitung linaeleza kuwa, kwa hakika, msaada huo hautoshi kwani, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa mataifa, zaidi ya watu milioni 25 ambao ni zaidi ya nusu ya idadi jumla ya watu wa Sudan, wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa.

Wataalamu wameshatahadharisha kuwa, kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, huenda kukawa na vifo visivyopungua milioni 2.5 kote nchini humo kutokana na njaa. Taifa hilo linakabiliwa na mzozo ulioibuka kati ya jeshi rasmi na kikosi kilichoasi cha RSF tangu mwezi Aprili 2023.

Kuwafikia Wasudan wanaokabiliwa na njaa ndiyo suala muhimu katika mazungumzo ya Sudan yanayofanyika mjini Geneva yaliyoanza Agosti 14 chini ya mjumbe maalumu wa Marekani Tom Perriello. Serikali ya Sudan iliahidi kuufungua mpaka wa Adre ambapo kikosi cha RSF kiliahidi kutoa ushirikiano katika uwasilishaji wa misaada ya kiutu.