1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika

Angela Mdungu
5 Julai 2024

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii ni pamoja na hatua ya waasi wa M23 kuviteka vijiji kadhaa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4hutg
Magazeti ya Ujeruman
Magazeti ya UjerumaniPicha: Hartmut Schmidt/imageBROKER/picture alliance

die tageszeitung

Moja ya habari kubwa Afrika iliyogonga vichwa vya magazeti hapa Ujerumani mwanzoni mwa juma ni hatua ya waasi wa M23 kuviteka vijiji kadhaa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. die tageszeitung liliandika kuwa, kitendo hicho kimewapa waasi hao mafanikio makubwa zaidi kwa mwaka huu.

Walikiteka kijiji cha Kanyabayonga walichokuwa wamekizingira. Hatua hiyo imetoa mwanya kwa kundi hilo la waasi kupata njia ya kupenya katika sehemu yenye idadi kubwa ya watu katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Jumamosi iliyopita, waasi hao wa M23 pia walifanikiwa kuudhibiti mji jirani wa Kibumba na vijiji vingine  huku wakiwaahidi wakaazi usalama na amani. Raia walioshuhudia miji hiyo ikitawaliwa walisema kuwa waasi hao walifika katika eneo la Kaseghe kilomita 100 kutoka Butembo ambao ni mji wa pili kwa ukubwa katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Die tageszeitung linaeleza zaidi kuwa, kwa sasa, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Tshisekedi analazimika kujilinda si tu kijeshi bali pia kisiasa. Katika serikali yake ya sasa, rafiki yake asiye na historia yoyote ya masuala ya jeshi alichukua nafasi ya aliyekuwa waziri wake wa ulinzi Jean-Pierre Bemba, kiongozi wa zamani wa waasi. Gazeti hilo linamalizia kwa kuandika kuwa, tangu wakati huo, kumekuwa na sintofahamu ndani ya jeshi la Kongo na sasa, jeshi limepoteza baadhi ya maeneo muhimu bila hata kuonesha upinzani na kumuaibisha Tshisekedi

Zeit Online

Zeit Online liliyamulika maandamano nchini Kenya. Licha ya kuondolewa kwa sheria tata ya kodi, yalifanyika maandamano dhidi ya serikali ya Rais William Ruto. Gazeti hilo la mtandaoni limeandika kuwa,  polisi walitumia mabomu ya machozi kuyatawanya makundi madogo ya waandamanaji. Kikosi kikubwa cha polisi kilifunga barabara zinazoelekea bungeni na katika makazi rasmi ya Rais wakati maduka yalilazimika kufungwa katikati ya  jiji la Nairobi.

Katikati ya mji wa Mombasa, mamia ya watu walikusanyika wakiwa wameshikilia bendera za Kenya na mavuvuzela pamoja na mabango yaliyomshinikiza Rais Ruto kung'atuka.  

Zeit Online limezinukuu takwimu zilizotolewa na tume ya haki za binadamu ya Kenya kuwa, katika maandamano hayo watu 39 waliuwawa. Kati ya hao ni kijana wa miaka 12.

Hali ya kiutu yazidi kuzorota Sudan
Hali ya kiutu ya Sudan ni mbayaPicha: Omer Erdem/Anadolu/picture alliance

Pia, watu  360 walijeruhiwa na wengine 32 hawajulikani walipo tangu yalipoanza maandamano hayo. Kulingana na gazeti hilo, maandamano hayo ndiyo yaliyotawaliwa na vurugu zaidi, tangu Kenya ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka 1963.

die tageszeitung

Habari kuhusu baraza jipya la mawaziri la Afrika ya Kusini zilitawala pia magazeti mengi ya Ujerumani, die tageszeitung lilijikita katika namna baraza hilo lilivyo na mchanganyiko wa mawaziri wenye misimamo tofauti ya kisiasa, weupe kwa weusi.

Liliandika, zaidi ya mwezi mmoja baada ya uchaguzi wa Afrika ya Kusini, Rais Cyril Ramaphosa ameitambulisha serikali yake mpya ya mseto. 

Chama cha ANC kililazimika kutafuta washirika ili kuunda serikali. Wiki kadhaa za mgogoro kuhusu nafasi za uwaziri kwenye serikali hiyo mpya zimefikia kikomo. Mgogoro huo umetatuliwa kwa kuundwa kwa baraza kubwa  zaidi la mawaziri katika historia ya Afrika Kusini lenye  mawaziri na manaibu waziri 75.

Neuer Zürcher Zeitung

Kwa upande wake  Neue Zürcher liliandika pia juu ya baraza hilo la mawaziri. Kubwa likiwa ni uteuzi wa waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika Kusini, Ronald Lamola wa chama tawala cha ANC. Lamola ana miaka 40.

Linabainisha kuwa kuiweka wizara hiyo chini ya ANC kunaashiria serikali ya Afrika Kusini kuendelea kuwaunga mkono Wapalestina na ukosoaji mkubwa wa taifa hilo dhidi ya harakati za Israel katika ukanda wa Gaza.

Gazeti la Die Zeit

Gazeti la Die Zeit, liliitupia jicho hali ya kiutu inavyoendelea kuzorota Sudan. Lilibainisha kuwa,  mamilioni ya watu wako hatarini kufa kwa sababu njaa inatumika kama silaha. Mhariri wa habari hii ameandika, wakati mwingine mtu anaweza kuamua kuziba masikio, lakini kwa bahati mbaya, kwa hali ya Sudan hilo haliwezekani. Ulaya inaweza na inapaswa kufanya kitu kubadilisha kinachoendelea nchini humo.

Zaidi ya watu milioni kumi wamelazimika kuyahama makazi yao, karibu 150,000 wameshauwawa na mji mkuu umeharibiwa vibaya. Miundo mbinu imeharibiwa au imeporwa. Hiyo ndiyo hali ya Sudan baada ya miezi 14 ya vita kati ya jeshi rasmi na kundi la RSF.

Hali ya kiutu yazidi kuzorota Sudan
Hali ya kiutu ya Sudan ni mbayaPicha: Omer Erdem/Anadolu/picture alliance

Siyo kwamba hakuna anayeingilia kati mzozo huu. Zaidi ya mataifa sita yanahusika kuchochea vita. Mengi kati ya hayo ni marafiki wa zamani ambao wameshachochea mizozo Yemen na Syria: Kulingana na Die Zeit, mataifa hayo ni  Saudi Arabia, Iran, na Misri yakiwa upande wa jeshi la Sudan.  Falme za kiarabu  inatajwa na ripoti za Umoja wa Mataifa kuhusu usambazaji wa silaha kuwa mshirika muhimu wa kibiashara wa kundi la RSF.

Taifa hilo linafahamika Ujerumani na Ulaya kuwa kituo muhimu cha gesi asilia na mashirika yake bora ya ndege. Hata hivyo Ulaya inapaswa walau kuiwekea vikwazo katika suala zima la usambazaji silaha na kusambaratisha taswira ya nchi hiyo iliyojijengea kama kisiwa cha anasa katika ulimwengu uliojaa vurugu. Hii ni kwasababu, jeshi la Sudan na kundi la RSF hawatafanya mazungumzo kama wanaendelea kupata fedha na silaha.