1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Josephat Charo
29 Januari 2022

Mapinduzi nchini Burkina Faso yamewashughulisha kwa kiwango kikubwa wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii. Kufunnguliwa kwa shule Uganda kumezingatiwa.

https://p.dw.com/p/46G7A
Symbolbild Pressespiegel
Picha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Mapinduzi Burkina Faso: Imekuwa taswira ya kawaida ya kutia wasiwasi katika eneo la Afrika Magharibi. Ndivyo lilivyoandika gazeti la Die Zeit. Mhariri aliandika kuhusu jinsi kundi la maafisa wa jeshi walivyotangaza kwenye runinga kupinduliwa kwa serikali ya kiraia, kusitishwa ka katiba na amri ya kutotoka nje.

Haya ni mambo yaliyotokea siku ya Jumatatu nchini Burkina Faso, nchi ya tatu baada ya Mali na Guinea, kukumbwa na mapinduzi ya kijeshi katika kipindi cha miezi michache tu. Rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia Roch Marc Kabore yuko kizuizini.

Mhariri wa gazeti la Die Zeit amesema Umoja wa Mataifa, Ufaransa na Ujerumani wanaingalia hali ilivyo katika nchi za Mali na Guinea, wakitafakari wasijue cha kufanya, kwa kuwa mataifa hayo ni muhimu sana katika vita dhidi ya ugaidi kwenye ukanda wa Sahel, vita ambavyo vimekuwa vikiongozwa na Ufaransa tangu mwaka 2013.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliandika kuhusu viongozi wa Ulaya kuondoka Afrika Magharibi na kutishia kuacha ombwe ambalo Urusi huenda ikalijaza. Mwandishi wa gazeti hilo Michaela Wiegel ameandika kuwa Afrika Magharibi imekuwa uwanja wa mnyukano wa madaraka ya kisiasa wa Urusi.

Baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso waandamanaji katika mji mkuu Ouagadougou walipeperusha bendera za Urusi. Hii ilinuiwa kuwa ishara kwa Wafaransa ambao jeshi lao limeendelea kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wakaazi.

Gazeti la Neuer Zürcher lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema: Mapinduzi katika ukanda wa Sahel ni matokeo ya umasikini. Mhariri alisema si jambo la kushangaza kwamba mapinduzi ya Burkina Faso yametokea, kwa kuwa hali ya usalama na uchumi katika eneo hilo ni mbaya. Nchi tatu za Sahel, ikiwemo Mali, Chad na Burkina Faso zimekumbwa na mapinduzi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Shule zafunguliwa Uganda

Nchini Uganda, kufungwa kwa muda mrefu kabisa kwa shule ulimwenguni kote kumeacha makovu makubwa. Ndivyo lilivyoandika gazeti la Neue Zürcher. Mwandishi wa gazeti hilo aliandika kwamba kufunguliwa kwa shule baada ya siku 660 Uganda kunadhihirisha athari kubwa na nyingi zilizotokana na hatua zilizochukuliwa kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Baada ya miaka takriban miwili hatimaye shule zilifunguliwa na kwa mujibu wa serikali hatua ya kuzifunga shule ilichukuliwa mwezi Machi 2020 kupunguza kitisho cha maambukizi ya corona kutoka kwa wanafunzi hadi kwa wazazi wao. Kwa upinzani, hatua hiyo ilichochewa kisiasa. Gazeti limesema kitu kimoja ni bayana: kufungwa kwa shule kumeacha alama na kusababisha athari za muda mrefu. Kutafuta pia baadhi ya mafanikio Uganda iliyoyapata katika sekta ya elimu katika miongo iliyopita.

Maafa katika mashindano ya soka Cameroon

Majonzi katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika. Ni kichwa cha habari kilichoandikiwa na gazeti la Süddeutsche. Kwa sababu mashabiki wengi walitaka kuingia uwanjani kulitokea mkanyagano kabla mechi ya duru ya mtoano ya timu kumi na sita bora kati ya wenyeji Cameroon na Comoro. Watu wasiopungua wanane walikufa katika malango ya uwanja huo.

Mhariri anasema wakati uwanja wa Stade Omnisport Paul Biya ulipofunguliwa mwaka 2021, hakuna aliyedhani kwamba eneo hili katika mji mkuu Cameroon, Younde, lingekabiliwa siku moja na ukurasa mbaya wa majonzi katika historia ya soka. Uwanja huo umepewa jina la rais Biya ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 30, lakini matukio ya Jumatatu jioni yumkini yakahusishwa na janga hilo kwa muda mrefu; watu waliokufa, waliojeruhiwa nje ya malango ya uwanja huo, taharuki na mechi ya soka ya kombe la Afrika ambayo pengine haikutakiwa kuchezwa baada ya matukio hayo.

Corona yavuruga tamaduni Afrika

Gazeti la die Tageszeitung liliandika makala kuhusu jinsi janga la corona linazivyovuruga tamaduni za Afrika. Hakuna sherehe za harusi, wala mabibi. Mhariri alisema baada ya miaka miwili ya janga la corona ulimwengu uko katika mchakato wa kukabiliana na maisha mapya ya kutumia teknolojia ya kidigitali makazini na katika biashara. Lakini barani Afrika, hali mpya haionekani sana katika nyenzo mpya za kufanyia mikutano kama Zoom, Google Meet au Microsoft Teams, bali ni kutoweka kwa tamaduni za kale, zenye thamani kubwa ambazo sasa zinanyongwa na kuangamizwa na hatua za kudhibiti janga la corona.

(Presseschau Afrika)