1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia yaendelea kugonga Vichwa vya Habari

15 Januari 2016

Mzozo wa Libya,jinsi ukosefu tamaa unavyowatumbukiza vijana mikononi mwa Al Shabab na kutokomezwa maradhi hatari ya Ebola ni miongoni mwa mada za Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii

https://p.dw.com/p/1He7N
Shambulio la Al Shabab,Novemba mosi katika hoteli Sahafi mjini MogadaischuPicha: picture-alliance/dpa/Y. Warsame

Visa vya wizi na kunajisiwa wanawake vinavyosemekana vimefanywa na watu kutoka Moroko na Algeria ndivyo vilivyohodhi ripoti ya magazeti ya Ujerumani hii leo. Hata hivyo wahariri walimulika pia miongoni mwa mengineyo,mapigano ya Sirte nchini Libya,miaka mitano tangu alipotimuliwa muimla wa Tunisia Zein El Abidine Ben Ali,hali ya wakimbizi wa Somalia na kushindwa nguvu maradhi hatari ya Ebola Afrika magharibi.

Tuanzie lakini Libya ambako wimbi la mageuzi lililoanzia Tunisia mwaka 2011 mpaka leo linaitikisa nchi hiyo ya Afrika kaskazini. Gazeti la mjini Berlin,Die Tageszeitung linazungumzia uwezekano wa kutumika ndege zisizokuwa na rubani,pamoja na ndege nyenginezo za kivita dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislam huko Sirte,pindi juhudi za kimataifa za kuundwa serikali ya umoja wa taifa zikifanikiwa. Kinyang'anyiro cha kuwania madaraka hakijamalizika licha ya kuteuliwa Fayez al-Sarraj kuwa waziri mkuu mwishoni mwa mwaka uliopita. Katika wakati ambapo mjini Tunis kinyang'anyiro ni cha kuwania nyadhifa wizarani,viongozi wa serikali isiyotambuliwa kimataifa ya mjini Tripoli wanaendelea kupinga kile wanachokiita "ufumbuzi wa amani unaolazimishwa na Umoja wa Mataifa."Kwa kuwa baraza la usalama la Umoja wa mataifa na nchi jirani na Libya wameshatangaza kuiunga mkono serikali ya Sarraj iliyoundwa kutokana na juhudi za upatanishi za mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Martin Kobler,Nuri Busahmain wa baraza la taifa au bunge la Tripoli na washirika wake wa itikadi kali,anatumia turufu ya kuvikalia vituo muhimu mjini Tripoli na kuahidi ikilazimika kuwatumia wanajihadi kuzuwia jumuia ya kimataifa isiingilie kati nchini humo. Die Tageszeitung linamalizia kwa kusema hata kama jumuia ya kimataifa itafanikiwa kuingilia kati nchini Libya,hali hiyo haitamaanisha amani bali mwanzo wa vita dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislam IS. Linawanukuu wataalam wa masuala ya usalama wakisema IS wanazidi kujipanua na wamepania kuugeuza mji wa Sirte nchini Libya kuwa makao makuu yao ya utawala wao au Khalifa barani Afrika.

Umasikini na Ukosefu wa Matumaini ndio Sababu ya Vijana kujiunga na Al Shabab

Somalia pia imegonga kwa mara nyengine tena vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii.Mbali na shambulio la Al Shabab katika uwanja mdogo wa ndege wa Somalia ambapo magaidi wanane,wanajeshi wawili wa kisomali na raia mmoja wameuwawa,wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamemulika pia jinsi wanamgambo wa Al Shabab wanavyojitajirisha kwa jasho la wananchi wa kawaida wa Somalia na fedha wanazopokea kwa kuwateka watu nyara. Süddeutsche Zeitung limezungumza na kiongozi wa idara ya upelelezi ya wanamgambo wa Al Shabab -Aminiyat,anaejiita Zamzam Adan Abdullahi anaesimulia yanayomfika mtu akikwepa kwa mfano kulipa "ushuru wa lazima" kwa Al Shabab.Yeyote mwenye kumiliki kitu analazimika kuwapaatia sehemu ya milki hiyo Al Shabab. Sio tu wenye kufanya biashara,bali mpaka wafugaji,mfano mwenye ngamia 20 anabidi awapatie al Shabab wawili. Anaelipa yuko salama anaekwepa kulipa anauliwa. Zamzam Adan Abdullahi anaelezea jinsi alilazimika kujiunga na Al Shabab: Alikuwa na miaka 12, alipolazimika kuacha shule kwasababu familia yake ilikuwa haina pesa. Umaskini na ukosefu wa matumaini ndio sababu ya vijana wengi kuamua kujiunga na kundi hilo la kigaidi linamaliza kuandika Südedutsche Zeitung.

Ebola yaatokomezwa Afrika Magharibi

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusiana na juhudi za kuyatokomeza maradhi hatari ya Ebola. Lilikuwa gazeti la Der Tagesspigel lililoripoti jinsi dawa ya kupambana na homa ya Malaria ilivyosaidia kumtibu mgonjwa wa Ebola. Tukio hilo limejiri wakati ambapo shirika la afya la kimataifa WHO limetangaza mwisho wa maabukizo ya homa ya Ebola katika eneo la Afrika magharibi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir:BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri: Daniel Gakuba