1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy akiri uhalifu wa kivita Tigray

23 Machi 2021

Kwa mara ya kwanza kabisa, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amekiri kuwepo kwa majeshi ya Eritrea katika jimbo la Tigray pamoja na kutendeka kwa matendo mabaya kabisa ukatili kwenye eneo hilo la kaskazini,

https://p.dw.com/p/3r0Yy
Äthiopien Abiy Ahmed
Picha: Amanuel Sileshi/AFP

Akizungumza mbele ya bunge hivi leo (Machi 23) mjini Addis Ababa, Abiy Ahmed amesema kwamba ripoti zinaonesha kwamba unyama mkubwa ulitendeka, akirejelea kauli yake ya kabla ya vita kati ya jeshi lake na wapiganaji wa kundi la TPLF kuanza kwamba: "Vita ni jambo chafu."

"Tunaujuwa uharibifu uliosababishwa na vita hivi. Wanajeshi waliwabaka wanawake." Aliongeza mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel huku akiapa kwamba "wanajeshi wote waliotenda matendo hayo na mengine ya uhalifu wa kivita watawajibishwa."

Hata hivyo, alisema kulikuwa na propaganda kubwa iliyoendeshwa na chama cha TPLF, ambacho kiliwahi kutawala jimbo la Tigray na ambacho viongozi wake wanaotafutwa sasa walipinga uhalali wa Abiy baada ya kuahirisha uchaguzi mwaka jana kutokana na janga la virusi vya corona.

Akiri kuwepo jeshi la Eritrea

Äthiopien Konflikte
Kimoja kati ya vifaru vya jeshi la Ethiopia vilivyotumwa kwenye vita vya jimbo la Tigray.Picha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Kwenye hotuba hiyo, waziri mkuu huyo pia alikiri kwamba vikosi vya jeshi la nchi jirani ya Eritrea viliingia Tigray kwenye mzozo huo uliochukuwa miezi mitano sasa.

Huu ni msimamo tafauti kabisa na ule wa kukanusha uwepo wa jeshi la Eritrea ndani ya ardhi ya Ethiopia, ambao serikali za mataifa yote mawili zilikuwa nao hadi hivi karibuni. 

Kwa mujibu wa Abiy Ahmed, vikosi hivyo viliingia mpakani kwa sababu Eritrea ilihofia kuwa ingelivamiwa na vikosi vya Tigray, akiongezaa kwamba serikali mjini Asmara iliahidi kuwaondowa wanajeshi wake mara tu jeshi la Ethiopia litakapoweza kurejesha udhibiti wa mpaka.

Mashirika ya kimataifa yataka uchunguzi huru

Weltspiegel 01.03.2021 | Äthiopien Tigray | Trauer um Toten
Vijana wakilia baada ya mwenzao kupigwa risasi na kuuawa kwa kuvunja marufuku ya kutembea na vikosi vya jeshi la Ethiopia katika mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle, siku ya tarehe 27 Februari 2021.Picha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Kauli hii ya Abiy imetoka muda mchache baada ya wakuu wa mashirika tisa ya Umoja wa Mataifa pamoja na maafisa wengine kutaka kusimamishwa mara moja mashambulizi dhidi ya raia katika jimbo hilo, ukiwemo ubakaji na aina nyengine za kuogofya za mashambulizi ya kingono. 

Kwenye taarifa yao, mashirika hayo, mchunguzi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na haki za binaadamu wa wakimbizi wa ndani na jumuiya mbili zinazowakilisha makundi ya kiraia yanayofanya kazi za kibinaadamu, yalitaka uchunguzi huru ufanyike ukihusisha Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa. 

Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yanaamini kwamba kilichotokea kwenye jimbo la Tigray kinakaribiana na kampeni ya mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Watigray, iliyowahi kuwa na nguvu sana kwenye siasa, jeshi na utawala wa Ethiopia licha ya kuwa wachache.