1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

2021: Mwaka mapidunduzi ya kijeshi yaliporejea Afrika

28 Desemba 2021

Mwaka 2021 umeshuhudia mapinduzi manne ya kijeshi yaliofanikiwa barani Afrika - katika mataifa ya Chad, Mali, Guinea na Sudan, idadi hii ikiwa imepanda kutoka tukio moja mwaka 2020.

https://p.dw.com/p/44vmw
Kombobild Präsidenten Mamady Doumbouya Guinea Mahamat Idriss Deby Tschad und Assimi Goita Mali

Akiwa amezungukwa na wanajeshi huku akiwa amejizungushia bendera ya Guinea mabegani, Kanali Mamady Doubouya alionekana kwenye televisheni ya taifa saa chache baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi mwezi Septemba.

Guinea ni nchi nzuri, aliwaambia makomredi wenzake, akielezea kile ambacho kingekuwa dira yake kwa ajili ya mustakabili wa taifa hilo, na kusema hawataki kuipora bali kuihudumia.

Awali vikosi maalumu vya Doumbouya vilivamia kasri la rais na kumtia mbaroni rais Alpha Conde, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo, na ambaye ushindi wake wa mwaka 2010 ulitazamwa kama mwanzo mpya baada ya miongo kadhaa ya utawala wa kiimla.

Soma pia: Jeshi la Guinea lasema Conde yuko nyumbani na mkewe

Lakini muda wa rais huyo mwenye umri wa miaka 83 madarakani ulimalizika kwa namna ya kipekee, kwa picha za video zilizomuonesha akiwa amekaa kwenye kochi lenye vumbi, akiwa peku huku vifungo vya shati lake vikiwa wazi na akizungukwa na walinzi waliojihami kwa silaha nzito.

Guinea | Fernsehansprache Mamady Doumbouya
Kiongozi wa kijeshi wa Guinea Mamady Doumbouya, siku alipotangaza mapinduzi ya utawala, Septemba 5, 2021.Picha: Radio Television Guineenne/AP Photo/picture alliance

Mapinduzi ya Spetemba 5 nchini Guinea hayakuwa utwaaji madaraka wa mwanzo wala wa mwisho wa kutumia nguvu mwaka huu barani Afrika. 

Hivi karibuni zaidi, jeshi la Sudan liliwakamata viongozi wa kiraia nchini humo na kutwaa madaraka mwezi Oktoba, karibu mwezi mmoja baada ya mamlaka kusema zilikuwa zimetibua njama ya mapinduzi walioilaumu kwa wanajeshi watiifu kwa mtawala wa zamani Omar al-Bashir.

Mnamo mwezi Mei, wanajeshi wa Mali walifanya mapinduzi yao ya pili katika muda wa miezi 10.

Hili lilikuja wiki kadhaa baada ya Jenerali Mahamat Idriss Deby kuchukuwa madaraka mara moja baada ya kusitisha katiba na kuvunja bunge kufuatia kifo cha baba yake akiwa katika uwanja wa vita.

Mapinduzi ya kijeshi yarejea baada ya kupungua pakubwa

Katika nusu ya pili ya karne ya 20, mapinduzi ya kijeshi barani Afrika yalitumiwa kama njia ya kawaida ya kubadili mifumo ya kisiasa baada ya uhuru.

Kati ya mwaka 1960 na 2000, idadi jumla ya mapinduzi na majaribio ya mapinduzi ilikuwa wastani wa nne kila mwaka, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jonathan Powell, Profesa mwandamizi katika chuo kikuu cha Central Florida, na Clayton Thyne, profesa wa chuo kikuu cha Kentucky.

Mali | Übergangspräsident Oberst Assimi GOÏTA
Kiomgozi wa kijeshi wa Mali, Assimi Goita.Picha: Präsidentschaft von Mali

Hata hivyo, wakati miito ya mageuzi ya kidemokrasia na utawala wa kikatiba ilipoongezeka katika karne mpya, mapinduzi ya kijeshi yalipungua hadi mawili kwa mwaka hadi mwaka 2019. 

Hivi sasa lakini, yanaonekana kurejea tena -- hali iliyomlaazimu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mapema mwaka huu, kulaani kile alichokiita "janga la mapinduzi ya kijeshi."

Wachambuzi wanasema ongezeko la karibuni la wanajeshi kujihusisha katika siasa kunashawishiwa na mchanganyiko wa vichochezi vya nje, ikiwemo kuongezeka kwa mataifa ya kigeni yanayotoa kipaumbele kwa maslahi yao, pamoja na masuala ya ndani, kama vile kukosa matumaini kwa umma dhidi ya rushwa, ukosefu wa usalama na utawala mbaya.

Umoja wa Afrika na jumuiya za kikanda kama vile jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWA zilisitisha uachama wa mataifa yalikofanyika mapinduzi isipokuwa Chad -- katika juhudi mza kuwalazimisha watawala wa kijeshi kujadiliana na viongozi wa kiraia. Lakini hatua kama hizo zimekuwa na athari kidogo.

Chanzo: Mashirika