1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

2020: Ongezeko la mauaji yanayolenga waandishi habari

29 Desemba 2020

Waandishi wa habari wapatao 50 wamepoteza maisha wakiwa kwenye kazi zao ndani ya kipindi cha mwaka 2020 kwa mujibu wa shirika la kutetea waandishi na vyombo vya habari duniani, Reporters Without Borders.

https://p.dw.com/p/3nJNh
Reporter ohne Grenzen | Cédric Alviani, Taipeh Bureau Director
Picha: Naomi Goddard/Minim Photo Studio

Kwenye mazungumzo mafupi kwa njia ya video na DW, mkuu wa Kamati ya Usalama wa Waandishi wa Habari ya Afghanistan, Najib Sharifi, amesema kwamba nchi hiyo haijawahi kuwa ya kuogofya kama ilivyo sasa, kwani kwa sasa kila mwandishi wa habari yuko hatarini.

Ndani ya kipindi cha wiki sita, Afghanistan imeshapoteza waandishi wanne wa habari, na wote ama waliuawa kwa risasi au kwa mabomu yaliyotegeshwa kwenye gari zao.

Hali ni hivyo hivyo kwenye maeneo mengine ya ulimwengu, kwa mujibu wa Shirika la Waandishi wa Habari Wasiokuwa na Mipaka, RSF, katika ripoti yake hiyo ya pili kutolewa.

Ingawa idadi ya waandishi wanaouawa wakiwa wanaripoti matukio ya mapigano imepunguwa, wale wanaouawa kwa kudhamiriwa imeongezeka maradufu.

Arubaini kati ya waandishi 50 waliouawa mwaka huu, wamekufa kwa kulengwa kwa makusudi na watu wenye silaha.

Mtangazaji wa kituo cha televisheni nchini Afghanistan, Malala Maiwand, aliuawa mapema mwezi huu wa Disemba, katika mashambulizi ambayo kundi lijiitalo "Dola la Kiislamu" lilidai kuhusika.

Lakini Sharifi anasema kwamba si rahisi kuwatambuwa wahusika na malengo yao. Zamani Taliban na kundi hilo la "Dola la Kiislamu" walikuwa wakibebeshwa tuhuma za mauaji kama hayo, lakini sasa tangu Taliban na serikali ya Afghanistan kuanza mazungumzo ya amani ni vigumu kumtambuwa muhusika.

Waandishi wa habari wanakabiliwa na vitisho na mashambulizi kutoka makundi ya wahalifu

Uganda | Journalisten am Uganda Media Center
Picha: Lubega Emmanuel/DW

Ripoti hiyo inaonesha kwamba kwa mara nyengine tena Mexico imeshika nafasi ya juu miongoni mwa mataifa yaliyo hatari sana kwa waandishi wa habari, ambako waandishi wanane waliuawa mwaka huu wakati wakichunguza matukio ya uhalifu wa kupanga na ufisadi.

Iraq ilipoteza waandishi watatu wa habari ambao walikuwa wakiripoti maandamano ya umma dhidi ya serikali mwezi Januari, ambapo mmoja kati yao alilengwa kwa makusudi na watu wenye silaha ambao walitaka kuvizuwia vyombo vya habari visiripoti maandamano hayo.

Nchini Pakistan, mwandishi wa habari Zulfiqar Mandrani alikutikana ameshakufa mwezi Mei, huku mwili wake ukiwa na alama za kuteswa. Marafiki na wenzake kazini wanadai kuwa kifo chake kilitokana na uchunguzi aliokuwa akifanya juu ya kesi ya madawa ya kulevya ambayo inahusisha maovu yaliyotendwa na maafisa wa polisi.

India nayo imewekwa kwenye orodha ya mataifa matano yaliyo hatari kabisa kwa waandishi wa habari duniani. Tangu mwaka 2010, shirika hilo la kutetea waandishi limesajili vifo vya waandishi watano wa habari nchini India kila mwaka. Mwaka huu limesajili vifo vinne ambavyo vinahusishwa na makundi ya uhalifu wa kupanga.

Ugunduzi huu umethibitishwa na Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari Ulimwenguni, CPJ, ambayo inasema waandishi wa habari wa India wanakabiliwa na vitisho na mashambulizi kutoka makundi ya wahalifu na pia maafisa wa serikali. CPJ imetaka uchunguzi wa kina wa mauaji ya mwandishi wa habari Rakesh Singh, aliyeuawa kwa bomu mwishoni mwa mwezi Novemba.

Mapema mwezi huu, Iran ilimnyonga mwandishi wa habari mwenye maskani yake nchini Ufaransa, Ruhollah Zam, akiwa wa kwanza kunyongwa ndani ya kipindi cha miaka 30, kwa tuhuma za kuchochea maandamano dhidi ya serikali mwaka 2017 kupitia chaneli yake ya ujumbe mfupi kwenye mtandao wa Telegram. Ruhollah alitekwa akiwa ziarani Iraq na akafungwa jela nchini Iran.

Shirika la Waandishi wa Habari Wasiokuwa na Mipaka pia limesema kwamba kuna mamia ya waandishi wa habari waliopoteza maisha yao mwaka huu kutokana na maradhi ya COVID-19. Baadhi ya vifo hivyo vilihusiana na kazi zao za kuripoti, tatu kati yao vikiwa katika mataifa ya Urusi, Misri na Saudi Arabia, ambako waandishi wa habari walikamatwa wakiwa kwenye kazi zao na kisha wakafa kwa COVID-19 kutokana na kunyimwa ruhusa ya kupatiwa matibabu.