1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magenge ya wahalifu nchini Haiti yaua watu 12

19 Machi 2024

Magenge ya wahalifu nchini Haiti yameshambulia maeneo mawili ya kitajiri yaliyopo Port-au-Prince na kuwaua watu 12, Magenge hayo yametekeleza uporaji na wizi wa vifaa vya umeme na kuathiriri utoaji wa huduma za msingi.

https://p.dw.com/p/4dtGu
Haiti Port-au-Prince | Tatort mit Opfern von Ganggewalt
Watu wakiwa wamekusanyika baada ya shambulio lililofanywa na magenge ya wahalifu Port-au-Prince, HaitiPicha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

     

Magenge ya wahalifu nchini Haiti yameshambulia maeneo mawili yaliyopo kwenye mji Mkuu  wa Port-au-Prince na kuwaua watu 12, Makundi hayo ya wahalifu yalifanya pia matukio mengine ikiwemo uporaji, wizi wa vifaa vya umeme na kupelekea usambazaji hafifu wa huduma ya maji na umeme katika jiji hilo.

Soma zaidi: Haiti yaendelea kukabiliana na magenge ya uhalifu

Majira ya asubuhi katika maeneo ya Laboule na Thomassin yaliyopo katika mji mkuu wa Haiti wa Port-au-Princewatu wenye silaha walivamia makazi ya watu na kuwalazimisha watu kukimbia, vurugu hizo za makundi ya kihalifu ziliwafanya wakazi wa maneno hayo kuanza kuvipigia vyombo vya habari ili kupata msaada wa polisi.

Mpiga picha wa Shirika la habari la Associated Press amesema kwamba aliona miili ya watu wasiopungua 12 iliyotapakaa kwenye mitaa ya Pétionville, iliyoko chini kidogo ya barabara kuu ya makazi ya watu kwenye maeneo ya milimani ya Laboule na Thomassin.

Haiti ,Port-au-Prince | Wanajeshi
Wanajeshi wa Haiti wakiwa kwenye doria katika mitaa ya Port-au-Prince, HaitiPicha: Odelyn Joseph/AP/dpa/picture alliance

Soma zaidi: Umoja wa Mataaifa waonya juu ya hali mbaya nchini Haiti

Mpiga picha huyo anasema baada ya muda mfupi alishuhudia umati wa watu ukianza kukusanyika karibu na watu hao waliopoteza maisha barabarani, anasema watu katika maeneo hayo walipatwa na taharuki kwa yale waliyokuwa wanayashuhudia akitolea mfano mwanamke mmoja ambaye alianguka na kulazimika kushikiliwa na wengine baada ya kujua kwamba ndugu yake ni miongoni mwa wale waliopoteza maisha barabarani.

Mashambulizi hayo yanayotekekelezwa na magenge ya wahalifu yaliaza tangu Februari 29 mwezi uliopita, Mwanaume mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema ''huu ni unyanyasaji uliokithiri, Watu wa Haiti amkeni, anzeni kuchukua hatua, kaka zetu wanakufa , siwezi kuzungumza tena.''

Kwa upande wake Douse Titit ambaye ni mfanyakazi katika ofisi ya meya ya PetionVille amesema mashambulizi hayo yanayofanywa na magenge ya wahalifu yamewaacha njia panda.

Dominikanische Republik | Grenze zu Haiti
Wanajeshi wa Jamhuri ya Dominica wakiwaruhusu raia wa Haiti kuingia nchini humo kununua mahitaji maalum sokoni kufuatia hali mbaya ya kiusalama nchini HaitiPicha: Fran Afonso/REUTERS

"Tuliamka asubuhi hii na kuona miili ya watu wetu hapa Petionville. Petionville sio jamii ya aina hiyo ambapo watu wanauawa, na tuko hapa kuondoa miili kabla ya watoto kuanza kutembea kwenda shuleni na wachuuzi hawajafika."amesema Titit.

Mashambulizi yazidisha hofu Haiti

Mashambulizi ya hivi karibuni yameibu wasiwasi wa kutositishwa kwa ghasia licha ya waziri mkuu wa nchi hiyo Ariel Henry kutangaza karibu wiki moja iliyopita kuwa atajiuzulu nafasi hiyo mara tu baada ya kuundwa kwa baraza la mpito.

Magenge hayo ya uhalifu kwa muda mrefu yamekuwa yakimpinga Waziri Mkuu Henry, yakisema kuwa hakuwahi kuchaguliwa na wananchi na kwamba amechangia kuongeza umaskini.

Dominican|Raia wa Haiti
Raia wa Haiti wakiwa kwenye foleni ya kuvuka mpaka kuingia nchi jirani ya Dominican kukimbia hali mbaya ya kiusalama nchini mwaoPicha: Fran Afonso/REUTERS

Hoja hiyo inapingwa vikali na wakosoaji wanaoamini kuwa magenge hayo yana nia yao ya kutaka utawala na sio vinginevyo.

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Ulaya, Takriban watu 17,000 wameukimbia mji mkuu wa Port-au-Prince kwa wiki iliyopita, Mataifa jirani na Haiti tayari yameanza kuimarisha mipaka yao.

Mipango ya kutumwa kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ambayo iliwasilishwa na serikali ya Haiti katika baraza na kupitishwa miezi sita iliyopita bado haijaanza kutekelezwa.